Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia ameridhishwa na tathmini ya Mkutano wa
Mashauriano wa awamu ya kwanza wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART),
uliofanyika hivi karibuni.
Mkutano huo ulihusisha Kampuni ya Simon Group inayomiliki mabasi
ya UDA na wamiliki wa mabasi ya daladala jijini Dar es Salaam. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuungana ili
kuleta maendeleo katika sekta ya usafiri Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi
karibuni, kuhusu maendeleo ya sekta ya usafiri na majadiliano
yanayoendelea kufanyika wakati huu kuelekea katika mfumo mpya wa mabasi
yaendayo haraka,Waziri Ghasia aliunga mkono jitihada zote, zinazofanywa na
wadau katika sekta ya usafiri.
“Kwa jinsi ambavyo mfumo unatakiwa uendeshwe na kwa jinsi
zabuni zitakapotangazwa bila kuwa na umoja itakuwa ni vigumu Watanzania
kupata kazi,” alisema na kuunga mkono makubaliano ambayo yameshafikiwa baina ya
pande husika.
Ghasia alisema uzoefu unaonesha kuwa Watanzania, wamezoea
kufanya kazi mtu mmoja mmoja, hivyo basi wakati umefika kuwa na kampuni moja, itakayokuwa na nguvu
katika sekta ya usafirishaji.
“Imani walioijenga kwa kuungana italeta tija kubwa kiuchumi katika
sekta ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam na wengine nao wataiga,”
alisema Ghasia.
Alisema kuwa mfumo mpya, utakaokuwa unatumika katika
uendeshaji utakuwa wa kisasa zaidi na kwa mfumo wetu wa kuchukua nauli ndani ya
daladala, hautakuwepo tena, hivyo ni lazima kuwa kitu kimoja.
“Mimi ningefurahi sana kama huu mfumo ungeshikiliwa na Watanzania
kuliko wageni,” Waziri Ghasia.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania, wabadilike na kuacha
kufanya kazi kwa mazoea.
Ghasia alisema anaamini wawekezaji wa ndani, wana uelewa mzuri na
mfumo huu mpya, hasa kutokana na kushirikishwa kutoka mwanzo wa mradi hadi
kufikia sasa, kutokana na kujifunza mambo kadha wa kadha nje ya nchi.
“ Ninashukuru tumekuwa na wamiliki wa usafiri kutoka zoezi hili
linaanza, DARCOBOA tumeenda nao mapaka Bogota nchini Colombia na wameona namna
mfumo unavyofanya kazi,” aliongeza Ghasia.
Alisema kuungana kwao ni ishara na namna walivyojifunza nchini
Colombia, jinsi wenzao walivyohama kutoka mfumo tulionao sisi na kuingia katika
mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka.
“Wawekezaji wetu waliona namna mfumo ulivyo mzuri na rahisi katika
jiji lile, hivyo ni somo tosha kwa wamiliki wetu wa hapa nchini, nashukuru
wameliona hilo,” alisema.
No comments:
Post a Comment