TIBAIJUKA AELEZEA HISA MRADI WA KIGAMBONI


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema hisa ya asilimia 10 kwa fidia watakayolipwa wananchi wa Kigamboni kupisha ujenzi wa mji wa kisasa ni hiari.
Akizungumza jana kwenye mkutano na madiwani wa kata sita zinazofikiwa na mradi huo, watendaji wa kata na serikali za mitaa, Tibaijuka alisema pamoja na timu  yake kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa hisa za wananchi katika mradi huo, uamuzi wa kuwa na hisa au la utabaki kwa mwananchi na haitakuwa lazima.
Tibaijuka aliwataka viongozi na watendaji hao, kusaidia kutoa elimu ya wananchi kukatwa asilimia 10 ya malipo ya fidia kama hisa mwananchi ili kuwapa uhalali wa kuendelea kumiliki ardhi yao kisheria.
"Kama ninyi madiwani mmekubali kukatwa sehemu ya fidia kama hisa ili muwe sehemu ya umiliki wa ardhi, sasa kwanini msisaidie kuelimisha wananchi kukubali mpango huo wenye manufaa siku zijazo?
“Si sahihi viongozi kusema kila mtu achukue chake na ajijue mwenyewe wakati hatua ya serikali ya kuwataka wananchi kuwa na hisa kwenye mradi huo ina faida kwa wananchi,” alisema Profesa Tibaijuka.
Aidha Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile alimtaka Profesa Tibaijuka kuhakikisha wanawaeleza wananchi kwa kina fedha za hisa, zitaratibiwa na nani na wananchi watapata manufaa gani.
Tubaijuka alisema mchakato wa namna fedha hizo zitaratibiwa na taasisi itakayoratibu unafanyiwa kazi na watalaamu na kuwa watu wote watakaokubali fedha zao kukatwa kwenye hisa watapewa mikataba maalumu.
Aidha, Profesa Tibaijuka alisema kuanzia Agosti 24, mwaka huu, watafanya mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuzungumzia mradi huo ambao awamu ya kwanza utafanyika katika kata sita.

No comments: