HAWA NDIO VIONGOZI WAPYA WA CHADEMA KIGOMA


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza majina ya viongozi wa chama hicho Mkoa wa Kigoma watakaokiongoza kwa muda kujaza nafasi zilizoachwa na waliokuwa viongozi waandamizi ambao wamejiunga na Chama cha ACT.
Akitangaza majina ya viongozi hao ambao walichaguliwa na mkutano wa wanachama kutoka majimbo manane ya mkoa huo, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo Chadema Makao Makuu Benson Kigaila alisema kuwa viongozi hao watakaa madarakani kusimamia uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi za matawi hadi mkoa unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu. 
Kigaila aliwataja viongozi waliochaguliwa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Ally Kisala ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa Kigoma na Shaban Madede ambaye amechaguliwa kuwa Katibu wa Mkoa.
Akitoa taarifa hizo za uchaguzi kwa waandishi wa habari, Kigaila aliwataja viongozi
wengine waliochaguliwa kuwa ni Omari Gindi ambaye amechaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la Vijana (Bavicha) Mkoa, Vestina James kuwa Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Mkoa na Jeremia Misigaro amechaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa. 
Katika hatua nyingine kiongozi huyo amesema kuwa hakuna athari zilizojitokeza hadi sasa tangu kujiuzulu uongozi na kujiunga na chama cha ACT waliokuwa viongozi wa Chadema Mkoa wa Kigoma wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa, Jafari Kasisiko. 
Alisema kuwa hakuna athari kutokana na viongozi hao kuondoka wao bila kuwa na kundi ambalo limewafuata na hasa madiwani na viongozi wa vijiji na mitaa ambao ndiyo wenye watu na kwamba kuondoka kwa viongozi hao pekee kumekuwa na athari ndogo ya kiuongozi na si  kichama.
Kwa upande wake Mwenyekiti  mpya wa Chadema aliyechaguliwa, Kisala alisema kuwa
wanayo changamoto kubwa katika kutekeleza majukumu yao hasa kutokana na changamoto kubwa ya uhaba wa rasilimali fedha na ushindani na vyama vingine.

No comments: