MGOGORO WA ARDHI WAIBUKA MVOMERO


Mgogoro wa ardhi umeibuka katika Kitongoji cha Majichumvi katika Kijiji cha Wami Luhindo wilayani Mvomero, baada ya Maofisa Ardhi kuanza upimaji viwanja.
Upimaji huo unafanyika katika utekelezaji wa azimio la ukaguzi wa mashamba pori yaliyotelekezwa kwa zaidi ya miaka 30 na wamiliki halali wa mashamba hayo.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Michael Mayalla, alisema hayo hivi karibuni katika mkutano  wa pamoja  na wananchi wa kitongoji hicho, kuhusu hatma ya mashamba hayo.
Mayalla alisema ameshangaa kuona  watu wa ardhi wakipima mashamba yao huku  wakijua kuna wakulima na wafugaji walihamishiwa  humo  kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Alisema alipowauliza maofisa hao kuhusu suala hilo, alipewa kauli kwamba mashamba hayo yanamilikiwa na vigogo.
Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Mvomero, Majaliwa Jafari, alipoulizwa alisema kati ya 1980 hadi 1990, Serikali ilitenga ekari 60,000 za mashamba  kwa ajili ya kilimo cha nguvu kazi katika kijiji hicho.
Hata hivyo alisema baadhi ya mashamba  yalinunuliwa na baadhi ya  watu  ambapo mengi hayakuendelezwa.
Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ilitoa agizo la kutambua mashamba pori ili yafutwe na kuangalia nini cha kufanya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Wami Luhindo, Apolinali Kahumba, alisema katika kijiji hicho kuna vitongoji sita kikiwemo cha  Majichumvi, ambapo pia alilalamika kuwa kilichofanyika ni halmashauri kutoshirikisha uongozi wa kijiji, ndio kilichoibua mgogoro.
Alisema sheria inaruhusu vijiji kugawa eneo lake kupitia Mkutano Mkuu wa Kijiji na kama Serikali inahitaji eneo, ni lazima kijiji kishirikishwe.

No comments: