TANZANIA KINARA WA UDHIBITI UTAKATISHAJI FEDHA HARAMU

Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi barani Afrika, ambazo zimeimarisha mifumo yake ya ndani ya kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu.
Shirika linaloweka viwango vya kimataifa vya uimarishaji mifumo ya udhibiti wa fedha haramu la Financial Action Task Force, limesema Tanzania ambayo huko nyuma mifumo yake ilikuwa dhaifu, kwa sasa imekidhi viwango hivyo.
Ripoti ya Shirika hilo ilisema shirika limefikia uamuzi huo baada ya mwezi Mei mwaka huu, kuitembelea Tanzania kufanya tathmini yake kuona inavyotekeleza malengo iliyojiwekea na kubaini kuwa imekidhibiti viwango vyote.
Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Udhibiti wa Utakatishaji wa Fedha Haramu, Onesemo Makombe alisema jana  kuwa, kwa hatua hiyo wawekezaji wengi ambao walikuwa wanainyooshea kidole Tanzania, sasa watarudisha imani kwa nchi na wataleta miradi mingi nchini.
Pia alisema nchi wahisani na wadau wa maendeleo wa Tanzania ambao miaka ya nyuma waliiweka Serikali kiti moto kuhusu udhaifu wa mifumo hiyo, sasa wanaweza kulegeza misimamo yao hasa kwa misaada ambayo walipanga kuipunguza.
Makombe alikiri kuwa tathmini iliyofanywa mwaka 2009  na Umoja wa Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Nchi zilizo Kusini  na Mashariki mwa Afrika ulibaini kuwa Tanzania ilikuwa na mfumo dhaifu wa kudhibiti tatizo hilo.
Alisema kati ya vigezo 16 vilivyowekwa katika tathmini hiyo, hakuna hata kigezo kimoja ambacho Tanzania ilikidhi."Hii ni hatua kubwa tumepiga na kama nchi ni lazima tujivunie."
Alitaja sababu kubwa ya Tanzania kuwa na ripoti mbaya ni kutokana na sheria ya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa inasema itafanya kazi na Zanzibar, lakini wakati wakaguzi wanakuja walikuta  sheria hiyo inatumika Bara tu.

No comments: