KESI DHIDI YA WAUMINI WA MOROVIAN YAAHIRISHWA

Kesi inayowakabili waumini 29 wa Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki na Zanzibar,  lililopo Mwananyamala imeahirishwa hadi Septemba 4, mwaka huu kutokana na baadhi ya washitakiwa kutofika mahakamani jana.
Wakili wa upande wa utetezi, Hezron Mwakenja alidai mbele ya mahakama hiyo kuwa baadhi ya wateja wake wameshindwa kufika  mahakamani kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo ya kufanya mtihani.
“Ni kweli mheshimiwa,  mshitakiwa Lamek Semkoko, huyu ni mwanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu John kilichopo Buguruni leo ana mitihani hivyo hakuweza kufika mbele ya mahakama hii, lakini pia nina barua hapa inayojulisha kutohudhuria kwake.
“Pia naiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine ya karibu kwa kuwa mshtakiwa Leonard Sanga naye Agosti 13, mwaka huu atakuwa na mitihani chuoni hapo,” alidai Wakili Mwakenya.
Awali Wakili wa Serikali alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya  washitakiwa kusomewa hoja  za awali.
Kwa mara ya kwanza waumini hao walifikishwa mahakamani hapo  Julai 20, mwaka huu, wakikabiliwa na kosa la kupigana hadharani kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 26 iliyofanyiwa marekebisho 2012.
Washtakiwa hao ni Profesa  Milline Mbonile (68), Anna Mwakibinga (78), Monica Muyombe (32), Ipana  Mapasa (35), Anneth Mbwile (61), Conjesta Mbanda (27), Lilian Edward (20), Jestina Sochombe (51), Sarah Mbonile (56), Hebroni Kyejo (57), Rose Mwakasambula (27), Peter Edson (35), Rodina Semengo (54), Jeremiah Mwamanda (34), Catherine Mwandalima (25), Leonard Sanga (22), Vanilla Limo (19) na Baraka Simon (22).
Wengine ni Subiraga Seba (43), Emmanuel  Fumbo (64), Yohana Kihonza (34), Lameck Simkoko (26), Nicodemas Mwasikili (19), Enea Kamwela (64), James Mwakalile (53), Huruma Bernad (31), Andrew Mkisi (51) na Lewis Mwandemani (29).

No comments: