MLEMAVU MBARONI KWA DAWA ZA KULEVYA

Mkazi wa Vijibweni, Said Tindwa (36), mwenye ulemavu wa mguu anashikiliwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kufanya biashara ya kulevya kwa kutumia ulemavu wake wa mguu bandia.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova, alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi baada ya kuwekewa mtego na polisi.
"Taarifa za kiintelijensia zilizopatikana kupitia kwa raia wema ziliwafikia makachero wa polisi kuwa mtu huyo ambaye mguu wake wa kulia ni wa bandia amekuwa akiutumia vibaya mguu huo kwa kuficha dawa za kulevya," alisema.
Alisema dawa hizo alikuwa akiwauzia watumiaji ambapo kila kete moja alikuwa akiiuza kwa Sh 1,000. Anapokutana na mteja huchomoa mguu na kutoa dawa hizo akishauza anarudishia mguu wake.
"Mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti Mosi katika mtego maalumu uliowekwa na askari wa upelelezi wakati akizitoa dawa hizo alikokuwa amezificha kwenye mguu wa bandia na kuwauzia wateja," alisema.
Kova alisema uchunguzi wa awali unaonesha kwamba mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu hiyo kwa muda mrefu kabla ya kukamatwa.
Alisema aina ya dawa alizokuwa akiuza mtuhumiwa huyo ni kokeni, heroine na wakati mwingine bangi ambapo uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea na jalada la kesi hiyo litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali.
Alitoa onyo kwa watu wenye ulemavu kutotumia kigezo cha ulemavu kufanya uhalifu kwa makusudi, kwani wanawaharibia watu wengine wenye ulemavu ambao mara nyingi huonewa huruma na kutotiliwa mashaka.
Wakati huo huo, wanawake watatu wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao haramu wa nyara za serikali katika maeneo ya Mbagala Misheni.
Kova alisema polisi walifika eneo la tukio na kumkamata Wamael Mshana na alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na vipande sita vya meno ya tembo vyenye
thamani ya Sh milioni 49.
"Taarifa za awali zinaonesha kuwa mtuhumiwa huyo anashirikiana na Upendo Mshana (33) na Stella Daniel (17) na wote wamekamatwa," alisema.
Katika hatua nyingine, polisi inamshikilia  Venance Manyika (38), mkazi wa Mbagala Misheni  kwa tuhuma za kukutwa na ngozi ya chui kinyume cha sheria.

No comments: