SITTA AWAPUUZA UKAWA, ADAI WAJUMBE WALIOPO WANATOSHA

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amepuuza maoni ya viongozi wa wajumbe wa Bunge hilo wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutaka Bunge hilo lisitishwe.
Akizungumza na wawakilishi wa wafugaji waliofika ofisini kwake jana kutaka Bunge hilo liendelee na kujadili masuala yao, Sitta alisema Katiba mpya itapatikana.
Alisema Katiba mpya itapatikana na wajumbe waliopo bungeni wanatosha kuandaa rasimu ya Katiba mpya, hivyo waliosusa vikao na kuamua kupiga kelele nje waendelee tu.
"Nasema waliopo bungeni wanatosha kupata Katiba mpya, kuna mambo mengi sana ya kujadili, haiwezekani muundo wa Serikali ukawa sababu ya kususa vikao.
“Hatua hii ya wafugaji ni ishara kuna mambo mengi na leo (jana) nilikuwa na watu wa Jukwaa la Wahariri nao wameleta mapendekezo ya maombi yao katika marekebisho ya rasimu," alisema.
Pia alisema Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika Sura ya Pili ibara ya 10, inazungumzia   haki za wafugaji na kuwahakikishia wafugaji hao kuwa matatizo yao yanajulikana na kwamba kitakachofanyika ni kuiboresha ibara hiyo.
Wakizungumza katika mkutano huo na Sitta, wafugaji hao waliokuwa wanatoka mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa Kanda ya Kusini, wakati wengine walikuwa kutoka Mwanza, Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Geita kwa Kanda ya Magharibi, walisema wamechoka kuendelea na mapigano kati yao na wakulima kwa sababu ya ardhi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Kanda ya Kusini, Huruma Ole Kalaita, alisema nchi ilipata uhuru bila kumwaga damu, lakini migogoro ya ardhi imesababisha matukio ya kumwaga damu na ndiyo sababu wanaomba wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wajadili masuala yao.
"Lakini kuna hili pia la wawekezaji wanamaliza ardhi, ni kama tunataka kuruhusu ukoloni," alisema Ole Kalaita.
Naye Mwenyekiti wa CCWT, Kanda ya Magharibi, Kusundwa Wamalwa, pamoja na mambo mengine alisoma risala rasmi ya wafugaji hao na kueleza kuwa kuna haja Katiba mpya ikawatetea na kuwasihi wajumbe wanaowakilisha makundi ya wafugaji wawe makini.
"Njia pekee ya kutusaidia ni kutuweka katika Katiba mpya, kinyume cha hapo ni kuleta matatizo makubwa. Wajumbe wa Bunge la Katiba wawe na hofu ya Mungu, Katiba bora ndiyo italeta maisha bora kwa kila Mtanzania.
"Tunataka Katiba bora iweke maslahi ya wafugaji na kama rasimu hiyo haitazungumzia kuhusu haki za wafugaji hatutaipokea," alisema.

No comments: