MWANAUME AUAWA KWA KUCHOMWA NA MKUKI KIFUANI

Mkazi wa Kijiji cha Bubutole Mbuyuni, Dogani Lupondije (48) ameuawa kwa kuchomwa mkuki kifuani huku watu wengine saba wakijeruhiwa baada ya kuzuka mapigano kijijini hapo.
Mapigano hayo yalizuka baina ya wanakijiji wanaojiita wa asili wa Bubutole Mbuyuni, Kata na Tarafa ya Farkwa wilayani Chemba, mkoani hapa na wafugaji wa Kisukuma wanaochukuliwa kama wageni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime (pichani) alisema Agosti Mosi mwaka huu walipokea  taarifa kutoka katika kijiji cha Bubutole Mbuyuni  kuwa kuna mapigano ya wanakijiji.
Alisema waliambiwa mapigano hayo yanahusisha wanakijiji wa asili wa eneo hilo na wasukuma ambao wanadaiwa ni wageni jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Misime alisema wananchi waliojeruhiwa katika tukio hilo wanapatiwa matibabu katika Zahanati ya Kwamtoro na kwamba Polisi inawasaka Adamu Swalehe na Ally Ramadhani, wakazi wa kijiji hicho na mkoani Arusha baada ya ushahidi kuonesha walichochea vurugu hizo.
Alisema chanzo cha mapigano ni fidia itakayotolewa kwenye ardhi katika kijiji hicho kupisha ujenzi wa bwawa. Wenyeji wanahoji fidia hiyo kwanini wapewe wageni ambao ndio wafugaji wa Kisukuma.

No comments: