'MGONJWA WA EBOLA' ASABABISHA TAFRANI SHINYANGA

Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, kwa siku mbili mfululizo walikumbwa na kiwewe, baada ya kuenea uvumi kwamba kuna mgonjwa wa mwenye homa hatari ya ebola, aliyefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Taarifa za kuwepo kwa mgonjwa huyo, zilidai kuwa mgonjwa huyo alitoka katika moja ya mitaa ya Manispaa ya Shinyanga na  alikuwa akitokwa damu puani na mdomoni kabla ya kuzimia.
Akizungumzia hali hiyo jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Ntuli Kapologwe alisema mgonjwa huyo ambaye alikuwa akitokwa damu mdomoni na puani, alifika hospitalini hapo juzi na baada ya kufika wauguzi na madaktari walitaharuki.
Kwa mujibu wa Dk Kapologwe, mgonjwa huyo alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), huku baadhi ya wauguzi na madaktari wakimkimbia hali iliyotia hofu kwa baadhi ya wahudumu na hata wagonjwa hospitalini hapo.
Hata hivyo, Dk Kapologwe alisema baada ya uchunguzi wa awali, ilibainika kuwa mgonjwa huyo ana matatizo ya kutokwa damu mara kwa mara na hajaambukizwa virusi hao wa ebola.
Akielezea namna mkoa ulivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo uliokwishaua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi, Dk Kapologwe alisema waganga wakuu katika halmashauri zote sita za wilaya mkoani Shinyanga, wameshajiandaa.
Alisema wamekubaliana atakapogundulika mtu mwenye dalili za ugonjwa huo, taarifa itolewe mara moja katika ngazi ya mkoa, ambako kuna timu maalumu ya wataalamu iliyoandaliwa kushughulika na ugonjwa huo hatari.
Baada ya taarifa kutolewa kwa mujibu wa Dk Kapologwe, timu hiyo itathibitisha kama mgojwa ana dalili zote za ebola na taarifa kutolewa kwa umma.
Wakati ugonjwa huo ukisababisha kiwewe mkoani Shinyanga,   mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe ameshauri wakazi wa mkoa huo kuwa macho na tayari kutoa taarifa kwenye vituo vya afya vilivyo jirani waonapo mtu mwenye dalili  za ugonjwa huo.
Alitoa mwito huo kupitia kwa waandishi wa habari aliozungumza nao jana ofisini kwake mjini hapa, baada ya kuibuka taarifa kuwa Rwanda kulikuwa na mtu anayehisiwa kuwa na ebola.
Hata hivyo, Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes Binagwaho alisema juzi kuwa mwanafunzi mmoja wa Ujerumani aliyefika nchini humo akitokea Liberia,  alihisiwa kuwa na ugonjwa huo lakini baada ya sampuli ya damu yake kupimwa katika maabara za kimataifa, hakukutwa na ugonjwa huo.
Massawe alisema Mkoa wa Kagera unapakana na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na pia upo mwingiliano wa watu na shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema nchi jirani zikipata mlipuko wa ugonjwa huo, upo uwezekano wa kuvuka mipaka na kuingia mkoani Kagera, hivyo ni  wajibu wa kila mmoja kutoa taarifa akiona mtu anayedhaniwa kuwa na ugonjwa huo.
Dalili za ugonjwa huo unaoenezwa na virusi vya ebola ni pamoja na  kutokwa na damu sehemu mbali mbali za mwili, kuumwa na kichwa, mwili kuishiwa nguvu, maumivu ya misuli na hatimaye kifo.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa kugusa damu na majimaji ya mgonjwa pamoja na kugusa vifaa au nguo za mgonjwa.
Massawe alisema Kagera wamechukua hatua kwa kuweka mikakati kuhakikisha mlipuko wa ugonjwa  hauingii nchini  kupitia mipakani. 
Miongoni mwa halmashauri ambazo zimeelekezwa kuchukua hadhari kutokana na kuwa mpakani mwa nchi, ni wilaya ya Bukoba, Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara.

No comments: