SHAHIDI AELEZEA ALIVYOINGILIWA NA MGANGA WA JADI



Shahidi wa pili katika kesi ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mganga wa kienyeji, Yahaya Michael (34) ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi alivyoingiliwa kimwili na mganga huyo kwa madai kwamba atampatia dawa ya kupata mtoto.
Mwanahamisi Omary (26) alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma kuwa alimfahamu mganga huyo baada ya kusumbuliwa na tumbo la uzazi kwa muda mrefu.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Felista Mosha, Mwanahamisi alidai alikuwa akitibiwa ugonjwa huo bila ya kutoa taarifa kwa mumewe Edrick Elinezer. Alidai alitibiwa kwa miezi sita bila ya mafanikio.
Shahidi huyo alidai Aprili, mwaka huu, Michael alimwambia kuwa ana majini hivyo hawezi kupata mtoto na kumpatia dawa kwa ajili ya kunywa na kuoga.
Alidai mganga huyo alikuwa akimtibu nyumbani kwake lakini baadaye alihamishia ofisi yake katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Kigogo Luhanga na kudai kuwa mganga huyo alikuwa akipaka dawa katika uume wake na kumuingilia kimwili huku akiwa hajitambui kwa madai kwamba atamsaidia kupata mtoto.
Aliendelea kudai kwamba baada ya kutokuwa na mawasiliano kwa muda mrefu na mumewe, alipata taarifa kuwa mume wake alipigiwa simu na mganga huyo na kumtaka apeleke gari lake Toyota Rav4 lenye namba za usajili T 139 BSG maeneo ya Jangwani kwa kuwa majini ya mkewe yanataka mtoto.
Awali, Hakimu Juma alisema wadhamini wa mshitakiwa wanatakiwa kumtafuta mshitakiwa huyo na kumfikisha Mahakamani hapo, aliwatahadharisha wasipofanya hivyo kwa wakati watalipa faini ya Sh milioni sita kwa kila mmoja.
Michael alidaiwa Aprili 29, mwaka jana, maeneo ya Jangwani Wilaya ya Ilala, alijipatia gari aina ya Toyota Rav4 T 139 BSG lenye thamani ya Sh milioni 12 mali ya  Eliezer kwa njia ya udanganyifu. Kesi hito itasikilizwa  tena Septemba 18, mwaka huu.

No comments: