Mtu mmoja ambaye inadaiwa kinara wa kuua na kujeruhi wanawake
maarufu, wafanyabiashara na wenye vyeo katika ofisi mbalimbali jijini Arusha,
Adamu Mussa (30) mkazi wa Majengo Juu jijini Arusha ametiwa mbaroni.
Mtuhumiwa huyo ametiwa mbaroni juzi usiku na polisi na alipopekuliwa
nyumbani kwake alikutwa na bastola mbili
na risasi saba na amekiri kuhusika katika mauaji na kujeruhi wanawake
jijini Arusha.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Lebaratus Sabas,
alizitaja bastola mbili zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa moja ni aina ya
Browning iliyotengenezwa Jamhuri ya Czech yenye namba A 895936 na ilikutwa na risasi
saba.
Alisema bastola ya pili aliyokutwa nyumbani kwake ni aina ya
Lorsin yenye namba za usajili 379126 iliyotengezwa nchini Marekani ikiwa na
risasi tatu.
Sabas alisema uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa bastola aina ya Browning
ilikuwa mali ya Seleman Bakari Msuya (33) mkazi wa Sombetini
jijini Arusha ambaye silaha yake hiyo iliibwa baada ya gari lake kuvunjwa kioo siku za nyuma.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amewasihi
wanawake kuwa na moyo wa uvumilivu na kuacha vyombo vya ulinzi na usalama
kufanya kazi zake ili kuwabaini wale wote wanaohusika na mtandao wa mauaji ya
wanawake pamoja na mtoto.
Mulongo aliyasema hayo jana jijini hapa wakati alipokuwa
akizungumza na wanahabari wa vyombo mbalimbali ofisini kwake juu ya ujumbe
uliosambazwa kwenye simu mbalimbali kupitia mtandao wa Whatsapp kuhusu
kujitokeza kwa wanawake/wasichana leo kwa Mkuu huyo wa Mkoa ili kujua hatma yao.
Akizungumzia suala hilo
Mulongo alitoa rai kwa akinamama wote pamoja na wasichana kuwa watulivu
na kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama kuwafichua wale wote wanaofanya mambo
hayo.
Awali juzi watu saba
walikamatwa jijini Arusha kwa tuhuma za
kuhusika kwenye
mauaji ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwa wanawake pamoja na kusababisha kifo cha mtoto, Christen Nickos mwenye umri wa miaka
mitatu na nusu mkazi wa
Olasiti jijini hapa.
Kamanda wa Polisi Liberatus Sabas alisema watu wawili kati ya saba
ambao ni
Japhet Lomnyaki (25) mkazi
wa Sakina na Nehemia Kweka (34) mkazi wa
Ngaramtoni walifikishwa mahakamani juzi.
Huku Adam Mussa (30) mkazi wa Majengo, Tito Loomoni (25) mkazi wa
Shamsi, Joseph Loomoni (29) mkazi wa Shamsi, Abdallah Maglan (202) mkazi wa
Oldadai na Emmanuel Maglan (23) mkazi wa
Oldadai wakiwa wanaendelea kuhojiwa na polisi.
No comments:
Post a Comment