Suala la Mahakama ya Kadhi limeleta mjadala mkali katika
majadiliano na wabunge wameamua suala hilo lisiingizwe kwenye Katiba.
Mjadala huo mkali uliibuka katika Kamati namba Saba ilipojadili
sura ya Nne ya kwenye rasimu hiyo inayozungumzia juu ya uhuru wa imani ya dini
ambapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hassan Ngwilizi alisema baada ya mjadala
mkali wamekubaliana kutoingizwa kwenye Katiba.
“Changamoto kubwa iliyojitokeza ni wakati tukijadili suala la
Mahakama ya Kadhi kuna baadhi ya wajumbe walitaka liingizwe kwenye Katiba na
wakanukuu Katiba ya Zanzibar imeruhusu Mahakama hiyo lakini tukaona si kweli na
baada ya mjadala mkali tumekubaliana Mahakama ya Kadhi iwe nje ya Katiba,”
alisema.
Ngwilizi alisema jana kuwa Kamati yake imeshakamilisha upigaji
kura na akidi kutimia kwa kila sura kwa kupata theluthi mbili kwa upande wa
Zanzibar na Bara, wameondoa kipengele cha uraia pacha kwenye rasimu ya Katiba
na kupendekeza kutungwe sheria itakayoingiza uraia huo kwa kuzingatia mambo
muhimu ya utoaji wa uraia huo.
Alitaja maoni mapya yaliyozingatiwa kwenye Kamati yake kuwa ni
pamoja na ardhi kuundiwa sura yake na masuala ya serikali za mitaa lakini
akaongeza “suala la kuwepo machifu au chochote kuhusiana na machifu
hatukujadili”.
Juzi Umoja wa Machifu Tanzania uliwasilisha mapendekezo yao
wanayotaka yaingizwe kwenye rasimu ya Katiba ikiwemo watambuliwe na
washirikishwe kuanzia Serikali za Mitaa kwenye kupanga mikakati ya kijamii,
kuundwe Tume ya Utamaduni na lugha za asili zilindwe na
kuendelezwa.
Kuhusu vipengele vilivyobadilishwa alisema “tumeondoa serikali
tatu na kuweka muundo wa serikali mbili na chemba za Bunge tumetaka mbili kama
ilivyo sasa yaani Baraza la wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano”.
Naye Mjumbe Abdallah Bulembo kutoka kamati hiyo namba Saba alisema
kwenye muundo wa Bunge kulitokea ubishi mkali kwani wapo waliotaka wabunge
watano kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wakawakilishe Bunge hili kwenye
Baraza la Wawakilishi Zanzibar lakini baada ya mjadala mkali wakakubaliana
muundo wa mabunge mawili ubaki kama ilivyo sasa.
Alisema kulikuwa na mvutano mkali kwenye suala la ardhi na
kusisitiza “wengi waliipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kuweka sheria
kwamba kwenye kiwanja chako kukionekana madini unaweza kuuza asilimia 80 na
asilimia 20 inabaki kwa mwenye kiwanja hivyo anakuwa mmoja wa wabia…mtaona
bungeni suala la ardhi litakuwa na mjadala mkali na itachukua muda
mrefu”.
Mjumbe Kaika ole Telele alisema suala la mgombea binafsi lilileta
mvutano mkali na mwishowe wakakubaliana awepo kwani halina madhara na kuzuia ni
kuminya demokrasia kwani hata Marekani wameruhusu na hajawahi kushinda.
Alisema wamekataa mabunge matatu na kukubaliana mabunge mawili
kama ilivyo sasa na serikali mbili na kufafanua “suala hili tulijadili kwa siku
mbili na hawa wajumbe kutoka Zanzibar waliridhika tubaki na mabunge mawili
baada ya kuvutana sana…tumekubaliana pia Rais apunguziwe madaraka ya uteuzi,
asiteue wakuu wa mashirika na taasisi aishie kumteua Mwenyekiti wa Bodi
tu”.
Kuhusu wafugaji alisema wamekubaliana kuwe na ardhi ya wafugaji
ili waache kutangatanga na hata maeneo ya mapori ambayo hayana hata
digidigi yarudishwe kwa Rais na wapewe wafugaji ili watulie.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Bunge, Samia Suluhu Hassan
alisema Kamati ndogo ya Uongozi imeshafanyia kazi juu ya Mahakama ya Kadhi,
Uraia pacha na muundo wa Bunge baada ya kukutana na wataalamu katika maeneo
hayo na leo wanakutana na makatibu wakuu wa wizara za fedha kwa Zanzibar na
Jamhuri ya Muungano kujadiliana juu ya kamati ya pamoja ya fedha ya muungano.
No comments:
Post a Comment