RAIS AJAYE WA AWAMU YA TANO APUNGUZIWA MZIGO



Mrithi wa Rais Jakaya Kikwete, atakayepatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani, ameanza kuandaliwa makao yake Ikulu, yatakayomwezesha si tu kuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania tajiri, bali pia kuanza kazi bila viporo vya miradi ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Tayari, Rais Kikwete ameshatangaza azma yake ya kutaka kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania masikini na katika tangazo hilo alilolitoa hivi karibuni Marekani, alisema muda wake uliobakia Ikulu, kazi kubwa ni kuandaa misingi ili Rais ajaye, awe Rais wa Kwanza wa Tanzania tajiri.
Juzi katika kujenga misingi hiyo, Rais Kikwete alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya lami kati ya Magole hadi Turiani, mkoani Morogoro, alisema atahakikisha kila mradi wa maendeleo ulioanzishwa wakati wa uongozi wake, unamalizwa.
Barabara hiyo ya Magole mpaka Turiani, ina urefu wa kilomita 48.6 na itagharimu Sh bilioni 49.44.
“Tulipoahidi kuwa tutajenga barabara za lami ili kuunganisha mikoa na wilaya, watu wasiotutakia mema walitubeza...lakini sasa wenyewe wanaona nini tumekifanya,“ alisema Rais Kikwete mbele ya wananchi waliofurika eneo la Mvomero.
Rais alisema, barabara nyingi za lami zimejengwa baada ya kupata Uhuru mwaka 1961 na nyingi katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Nne ulioanza 2005.
“Wakoloni walituachia barabara chache za lami, kuja Morogoro kutoka Dar es Salaam na Dar es Salaam kwenda Tanga  pamoja na za mijini katika maeneo waliyokuwa wakikaa wazungu ...hizo zingine zote mnazoziona zimejengwa baada ya Uhuru,” alisema Rais kwa wananchi hao.
Aliendelea kusisitiza na kurudia kauli yake, kwamba atasimamia miradi ya barabara, umeme, maji ma mingine, ili imalizwe kabla ya kustaafu Urais na kama kutatokea ikabaki kwa bahati mbaya, basi iwe michache isiyokuwa mzigo kwa mrithi wake.
Rais alisema ziara yake ya Mkoa wa Morogoro ilipokuwa ikianza Agosti 20 mwaka huu, aliagiza apangiwe kwenda maeneo ambayo hayajafikiwa na viongozi wa kitaifa wa ngazi ya Rais.
Baada ya kufika katika maeneo hayo, ikiwemo Nyandira na Kibati katika Wilaya ya Mvomero, Kisanga na Msolwa katika Wilaya ya Kilosa na Kisaki na Kinole, katika Wilaya ya Morogoro, amejionea mwenyewe kasi ya maendeleo inayohitajika kupelekwa vijijini.
 “Bado nina muda, katika bajeti ijayo tunaongeza fedha katika miradi ya maendeleo, ili kuwezesha ifikie mwisho na kama itakuwa bado, basi iwe ni michache kuepusha mzigo kwa mrithi anayefuata,“ alisisitiza Rais Kikwete.
Hivi karibuni Rais Kikwete alipokuwa akizungumza  katika Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo mjini Washington DC, Marekani, alisema anataka na anatamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania, kuongoza nchi ambayo ni masikini.
Ili kutimiza lengo lake hilo, Rais Kikwete alisema atatumia muda wake uliobakia katika uongozi, kuelekeza nchi kwenye mwelekeo huo, ambao ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na gesi asilia.
“Rasilimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa kati ya sasa na
mwisho wa kipindi changu cha uongozi, ni kuiongoza nchi yetu kuelekea kwenye njia hiyo, ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora zaidi kwa wananchi wetu,” alisema.
Akimzungumzia Rais ajaye, Rais Kikwete akiwa Marekani, alisema ili Watanzania wanufaike na mapato ya gesi, ni muhimu kuwepo na uongozi imara, ambao utakuwa tayari kuchukua uamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyosonga mbele.
Alisema anataka kufanya kila linalowezekana katika kipindi chake kilichobakia cha uongozi, kuhakikisha anaanzisha na kuanza kujenga taasisi na kuweka kanuni sahihi za kusimamia rasilimali ya gesi asilia.
Tayari Serikali imeweka hadharani mapendekezo ya Sheria ya Mgongano wa Maslahi, ambayo itawalazimisha viongozi na watumishi wa umma,  kutenganisha uongozi pamoja na utumishi wao kwa umma na biashara, ili kuzuia ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma unaoendelea kutokea nchini.
Katika mapendekezo hayo yaliyoanza kujadiliwa na wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa sasa, viongozi wote  na watumishi wa umma, watatakiwa kuchagua kati ya mali na biashara zao na nafasi ya utumishi wa umma. 
Uchaguzi huo utafanyika kwa namna mbili; moja kukabidhi biashara zote kwa kampuni ya udhamini, ambayo itaziendesha biashara hizo huku mtumishi mwenye mali, akipewa taarifa chache kuhusu biashara yake kwa mwaka.
Pili mali na biashara ambazo kiongozi wa umma atakuwa nazo, ambazo zinaweza kusababisha mgongano wa maslahi, atatakiwa kuziuza kabla ya kukubali kazi ya kutumikia umma au kampuni ya udhamini, inaweza kuuza mali hizo bila hata kumpa taarifa.
Miongoni mwa viongozi wa kwanza kuzungumzia mapendekezo hayo, ni marais wastaafu; Mzee Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili na Benjamin Mkapa, wa Awamu ya Tatu.
Akizungumza sheria hiyo,  Mzee Mwinyi, alisema Azimio la Arusha, lililokuwa na miiko ya uongozi, iliyosimamia maadili ya viongozi wa umma halikufutwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, bali lilizimuliwa  ili kuwapatia viongozi uwezo wa kumudu makali ya maisha.
Alisema lakini tofauti na matarajio, viongozi walitumia vibaya nia njema ya Serikali kwa kuanza kumiliki mali hata kwa njia zisizo halali na kuongeza; “tuliwaruhusu kuingiza mkono, lakini wao wakaingiza mwili mzima.”
Naye Mkapa juzi alipokuwa akizungumzia mapendekezo hayo, alisema mtumishi au kiongozi wa umma anayedhani kuwa sheria hiyo ni kandamizi, huenda akawa na tatizo la kutumia vibaya mamlaka ya umma.

No comments: