OKWI AZICHEZEA AKILI SIMBA NA YANGA


Mshambuliaji matata wa Uganda Emmanuel Okwi sasa ni kama ameamua kucheza na akili za viongozi wa Simba na Yanga.\
Wakati juzi Rais wa Simba Evanse Aveva akisema hawana nafasi ya Okwi kwenye usajili wao, jana Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe alitangaza mchezaji huyo ameandika barua ya kuombwa kusajiliwa katika klabu hiyo ya Msimbazi nao wamemkubalia. 
Hata hivyo, Okwi ana mkataba na Yanga aliosaini nao Desemba 15 mwaka jana kwa  miaka miwili na nusu na juzi alikanusha tetesi kwamba anataka kujiunga na timu ya WadiGalde ya Misri akisema yeye ni mchezaji halali wa Yanga na bado ana mazungumzo mazuri na viongozi wake. 
“Watu wanazusha maneno kwamba nataka kwenda kucheza soka nje, nashangaa yanatoka wapi, mimi bado ni mchezaji halali wa Yanga,” alisema Okwi. 
Yanga imemshitaki Okwi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  ikitaka afungiwe kucheza soka kutokana na kukiuka baadhi ya vipengele kwenye mkataba wake likiwemo kufanya mazungumzo na klabu ya WadiGalde FC ya Misri. 
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jana, Okwi alisema hadaiwi chochote na Yanga kwani wao ndio waliovunja naye mkataba wakidai kuwa aliwakosesha ubingwa. 
“Yanga hawanidai, wao ndio walovunja mkataba na mimi, wakiniambia kuwa nimewakosesha ubingwa msimu uliopita, sasa wananidai nini,” alisema. 
Aidha Okwi alikiri kupata barua ya TFF ikimfahamisha kwamba Yanga imemshitaki, ambapo alisema yupo tayari kutoa ushirikiano katika hilo. 
Kabla ya kusajiliwa Yanga mwaka jana, Okwi aliichezea Simba kwa misimu mitatu na baadaye akauzwa Etoile du Sahel ya Tunisia ambapo hata hivyo hakufanya vizuri na kuamua kurudi kwao Uganda katika timu ya SC Villa. 
Okwi alirudi Villa kwa msaada wa Fufa (Shirikisho la Soka la Uganda) ambalo liliiomba CAF kumruhusu acheze kwa muda ili kulinda kiwango chake ambapo Shirikisho hilo la Soka la Afrika lilimruhusu kucheza kwa miezi sita, lakini kabla hajaitumikia akaibukia Yanga. 
Kitendo cha Yanga kumsajili Okwi kilizua utata Simba kwani ilimtoa mchezaji huyo Etoile bila malipo kwa makubaliano wangelipwa kwa awamu, mpaka sasa Simba haijalipwa fedha zao na kesi hiyo ipo Fifa. (Shirikisho la Soka la Kimataifa).

No comments: