SABA MBARONI KWA TUHUMA ZA KUPORA NA KUUA WANAWAKE

Watu saba wamekamatwa Jijini Arusha  kwa tuhuma za kuhusika kwenye mauaji ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwa wanawake.
Wanadaiwa pia kusababisha   kifo cha mtoto, Christen  Nickos mwenye umri wa miaka mitatu na nusu  mkazi wa Olasiti hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema watu wawili kati ya saba ambao ni Japhet  Lomnyaki (25) mkazi wa Sakina na Nehemia Kweka (34) mkazi wa Ngaramtoni walifikishwa mahakamani juzi.
Alitaja wengine, Adam Mussa (30) mkazi wa Majengo, Tito Loomoni (25) mkazi wa Shamsi, Joseph Loomoni (29) mkazi wa Shamsi, Abdallah Maglan (22) mkazi wa Oldadai na Emmanuel Maglan (23)   wa Oldadai wanaendelea kuhojiwa na polisi.
Alisema wanatuhumiwa kuhusika kwenye tukio la Agosti 21 mwaka huu maeneo ya Olasiti ambako wakiwa na pikipiki aina ya Toyo , walimjeruhi kwa kumpiga risasi mtoto Christen  sehemu ya mdomo na kusababisha kifo chake.
Wanatuhumiwa pia kuhusika kwenye tukio lingine la mauaji ya mwanamke Shamimu Yulu (30) maeneo ya Sakina  kwa Idd ambaye alipigwa risasi na kufariki dunia akiwa anapatiwa matibabu hospitali ya Selian.
Mwanamke mwingine Flora Porokwa alilazwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (Selian) baada ya kupigwa risasi ya bega kwenye tukio lingine tofauti likihusisha watu waliokuwa kwenye pikipiki.

No comments: