KITENGO CHAUNDWA TAKUKURU KUKABILI 'WALAFI'

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kukabili watu wenye madaraka serikalini wanaojilimbikizia mali isivyo halali.
Alisema vigogo watakaobainika kwa mujibu wa mahakama, mali zao zitataifishwa na kuzirejeshwa serikalini kwa manufaa ya umma.
Lengo la taasisi hiyo ni kuokoa mali zenye thamani ya mabilioni ya shilingi ambazo zinamilikiwa isivyo halali na baadhi ya viongozi ambao hawana maelezo ya kina ya jinsi mali hizo zilivyopatikana.
Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema hayo jana mjini Moshi kwenye kikao cha maofisa wa taasisi hiyo kutoka mikoa na kanda zote nchini. Kinalenga kutathimini utendaji kazi na maandalizi ya kustaafu utumishi wao.
Alisema iwapo viongozi watakuwa waadilifu Tanzania, ina uwezo wa kuwa na miundombinu bora, uimarishwaji wa sekta za afya, elimu, kilimo na uchumi unaokua kwa kasi.
Dk Hoseah alisema katika kujenga kizazi kijacho chenye uadilifu na nidhamu ya madaraka, taasisi yake imejikita katika kufungua klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi ambapo hadi sasa kuna klabu 2,371 zenye wanachama 172,706 katika shule zote za msingi nchini.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alisema serikali inathamini mchango mkubwa wa Takukuru katika kupambana na rushwa na kutaka wananchi kuunga mkono taasisi hiyo kwa kutoa taarifa kila wanapobaini kuwapo kwa mazingira ya rushwa.

No comments: