MATAJIRI WAJIMEGEA HIFADHI ZA MISITU

Baadhi ya matajiri wanadaiwa kujimegea maeneo ya hifadhi mbalimbali, ikiwemo maeneo ya hifadhi ya Mikoko jijini Dar es Salaam kwa kutumia ramani bandia.
Misitu mingine inayodaiwa kuvamiwa kwa mtindo huo ni wa Mikoko wa Delta ya Rufiji, Msitu wa Akiba na Nishati Morogoro/Mvomero, na Msitu wa Kazimzumbwi (Chanika).
Utafiti  wa hifadhi za misitu na mikoko nchini uliofanywa hivi karibuni na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya mazingira, umebaini ufisadi huo unaodaiwa kufanywa kwa kushirikiana na  watumishi wa serikali wasio waaminifu.
Ripoti ya utafiti huo ilitolewa wiki hii na T FS kwa waandishi  jijini Dar es Salaam ikielezwa kwamba  asilimia kubwa ya misitu nchini iko hatarini kutoweka ikiwa kasi ya uvamizi unaofanywa ndani ya hifadhi hizo hautadhibitiwa.
Msaidizi Misitu Mkuu wa TFS, Kanda ya Mashariki, Paul Ndahani alisema miaka 10 iliyopita wananchi walivamia misitu na kuiba miti, lakini hivi leo wananchi wengi wenye fedha (matajiri)  wamevamia misitu hiyo bila woga na kutengeneza mashamba na kisha kujenga nyumba.
“Hali ni mbaya, mfano mkoa wa Morogoro, wavamizi wa ardhi ya hifadhi ya msitu wa akiba wanatishia uhai wa hifadhi hiyo, matajiri wenye fedha wameingia ndani ya msitu na kujimilikisha zaidi ya ekari 300,” alisema Ndahani.
Alisema jitihada zao za kuwaondoa wavamizi hao zinakumbwa na changamoto kubwa ikiwemo vitisho, jambo ambalo linawawia vigumu kwa kuwa watu hao wanajulikana kwenye Halmashauri na hata mkoani.
Mtafiti Charles Kayoka aliyefanya utafiti wa uharibifu wa maeneo ya Hifadhi ya Misitu kwenye maeneo hayo nchini alisema, hali ni mbaya na jitihada za haraka zinahitajika kunusuru mazingira.
Alisema kwenye hifadhi ya Mikoko ya Dar es Salaam, hali ni mbaya kwani baadhi ya wananchi wamejimegea sehemu ya hifadhi hiyo bila kufahamu sheria zinazolinda eneo hilo na maeneo mengine baadhi ya watendaji wa serikali wasio waaminifu wamechora ramani bandia na kuwauzia watu viwanja.
“Hii tumeikuta hususan kwenye maeneo ya Bahari Beach, Ununio na Kinondoni Hanannasifu ambapo maeneo hayo wamo matajiri wenye tabia ya kujimegea hifadhi ya mikoko kwa kushirikiana na vishoka wanaochora ramani bandia,”alisema Kayoka.
Kayoka alisema zipo hatua zilizochukuliwa kwa baadhi ya maeneo ambayo serikali imeona uvamizi huo na kuanza kuvunja majengo yaliyojengwa na kwamba nguvu zaidi inahitajika kuwaondoa wavamizi hao hususan kwenye hifadhi za misitu.
Kutokana na hali hiyo, TFS na wadau wa mazingira  wameomba serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watendaji wote wa halmashauri na  watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Aidha alishauri halmashauri za Manispaa na wilaya nchini kuhakikisha watendaji wake wanafuata sheria na wanajifunza sera na sheria zote zinazohusu mazingira, ardhi na misitu ili wanapotaka kufanya maamuzi wazizingatie kwa pamoja.

No comments: