POLISI WASAMBARATISHA MAANDAMANO YA ALBINO DAR



Maandamano ya walemavu wa ngozi kwenda Kituo cha Polisi Buguruni jijini Dar es Salaam jana, yalisambaratishwa kwa mabomu ya machozi na askari Polisi, baada ya waandamanaji hao kuzingira kituo hicho na kukaidi amri ya kutawanyika.
Waandamanaji hao walitokea Mahakama ya Mwanzo Buguruni kwenda katika kituo hicho, kulalamikia uamuzi wa Mahakama hiyo kutoa dhamana kwa mshitakiwa, Ombeni Swai, mkazi wa Tabata Matumbi, anayedaiwa kutishia kumuua mwenzao.
Kabla ya maandamano hayo, Swai alifikishwa mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Benjamini Mwakasona na kushitakiwa kwa kosa la kutishia kumuua mlemavu wa ngozi, Mwinyisi Issa.
Karani wa mahakama hiyo, Edwin Mwandawanda alidai mahakamani hapo kwamba Swai alitishia kwa maneno kumuua Issa Agosti 16 mwaka huu, saa 7 mchana katika eneo la Buguruni Wilaya ya Ilala.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo ambapo Hakimu Mwakasona aliahirisha kesi hiyo mpaka Septemba 3, mwaka huu na kumwambia mshitakiwa kuwa dhamana ya kesi yake ipo wazi, ambapo alitakiwa kuwa wadhamini wawili waliotakiwa wote kuwa na barua zinazotambulika na serikali za mtaa.
Pamoja na dhamana hiyo kuwa wazi, mshitakiwa hakufanikiwa kutimiza masharti hayo kwa wakati, hivyo akaendelea kushikiliwa wakati akisubiri wadhamini wake kutekeleza masharti hayo.
Kitendo hicho cha mahakama kutangaza dhamana kwa mshitakiwa, kiliamsha hasira kwa walemavu wa ngozi waliokuwa wamekusanyika nje ya mahakama kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, iliyotajwa kwa mara ya kwanza.  
Baadhi ya walemavu hao walifanikiwa kupenya mpaka alipokuwepo mshitakiwa na kuanza kumpiga.
Kitendo hicho kilifanya Polisi kumpakia haraka kwenye gari na kumpeleka kituoni Buguruni, kwa nia ya kumnusuru.
Hatua hiyo haikuwaridhisha albino hao, ambao walijikusanya na kuandamana kwenda katika Kituo cha Polisi Buguruni, kwa lengo la kutaka kumdhuru mshitakiwa.
Mashuhuda waliozungumza na gazeti hili, walidai kuwa waandamanaji hao walipotakiwa kutawanyika,  walikaidi, hatua iliyosababisha Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Walisema  baadhi ya albino walidiriki kupanda ndani ya gari la polisi  aina ya Land Rover 'Defender' na kuanza kumshambulia kwa mateke na ngumi mshitakiwa, jambo lililowalazimu polisi kuondoka eneo hilo hadi kituo cha polisi Buguruni.
Albino hao pia walifuata kwa nyuma huku wengine walipanda ndani ya gari hilo hadi mahali hapo.
Wananchi waliokuwepo nje ya kituo cha polisi, walikumbwa kwa taharuki. Albino hao waliendelea kumshambulia mshitakiwa huyo hadi walipofika nje ya kituo hicho, huku wakizuiliwa na polisi hao, ambao baadae walilazimika kufyatua mabomu ya machozi  kwa lengo la kuwatawanya.
Mwandishi alimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marry Nzuki, ambaye alikiri kutokea kwa vurugu hizo. Alisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa Polisi kwa kosa hilo.
"Baada ya kutawanywa pale kituo cha Buguruni, Mkuu wa Kituo aliwaambia waje katika ofisi zangu, lakini hadi hivi sasa sijamuona mtu yeyote wala kiongozi wao kuleta mashitaka yoyote," alisema Kamanda Nzuki.
Wakati vurugu hizo zikitokea, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ametangaza kutoa Sh milioni 10 kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa watu walioshiriki kumkata mkono mlemavu wa ngozi, Susan Mungi (35) na kumuua mumewe wilayani Igunga, Tabora.
Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, Mengi alisema pia IPP itasomesha watoto wa mlemavu huyo.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), Mengi alisema anafanya hivyo kama mwananchi wa kawaida ambaye ameguswa na vitendo hivyo vya kinyama, vinavyofanywa dhidi ya watu hao wenye ulemavu.
Aliomba Polisi kuwasaka wote waliohusika, kuwakamata na kuwapeleka mahakamani haraka.
Alisema albino ni watu kama wengine hivyo vitendo vyovyote vya kinyama dhidi yao lazima vilaaniwe na watu wote.
"Hakuna albino ambaye amependa awe hivyo, hakuna aliyemwomba Mungu ampatie ulemavu huo, hawa ni binadamu kama sisi, jamii na serikali kuendelea kukaa kimya juu ya unyama huu ni jambo linalosikitisha," alisema Mengi. Mengi alisema waliotumwa kumkata albino huyo wakamatwe.
Susan, mkazi wa Kijiji cha Buhelele kati ya Nsimbo wilayani Igunga, alikatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho.
Katika tukio hilo, mumewe Mapambo Mashili aliuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha  kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.
Mtoto huyo hadi  sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo.  Katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora,  Fatma Mwasa ametangaza dau la Sh 500, 000 kwa mwananchi atakayesaidia kukamatwa kwa watu wanaofanya vitendo hivyo.
Tukio hilo limekuwepo ikiwa ni wiki baada ya mtoto, Upendo Sengerema (15) mkazi wa Kijiji cha Usinge kata ya Uganza wilayani Kaliua mkoani Tabora, kukatwa mkono na watu waliokimbia nao.
Katibu Mkuu Chama cha Albino (TAS), Ziada Nsemo alisema kati ya watanzania milioni 45, Mengi ni mmoja wa watu waliojitokeza hadharani kukemea vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa. Alisema licha ya polisi kuahidi kuwalinda, wameendelea kuuawa.
Alitoa mwito kwa albino nchini, kujilinda na kukaa karibu na makundi ya watu ili wanapovamiwa iwe rahisi kupata msaada kwa sababu ulinzi kwao ni wa shaka na wanawindwa kila kona.

No comments: