UTOAJI VITAMBULISHO VYA TAIFA WAKAMILIKA DAR NA ZANZIBAR


Kazi ya kuandikisha na kutoa vitambulisho vya Taifa, imekamilika Zanzibar na mkoa wa Dar es Salaam. 
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Thomas William (pichani) alipozungumza na mwandishi wa habari hizi. 
Alisema  kwa sasa wanakwenda mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara kwa ajili ya kuandikisha na kuchukua alama za vidole. 
Alisema wananchi  ambao hawakujiandikisha awali kwa ajili ya kupata vitambulisho vya taifa katika mikoa ambayo mchakato huo umekamilika, wanatakiwa kwenda kwenye ofisi za NIDA za wilaya na tarafa kukamilisha shughuli hiyo. 
Alisema wananchi ambao hawakujiandikisha katika mikoa hiyo ambayo mchakato wake umekamilika,  wanayo nafasi ya kufanya hivyo. 
Alisema mwananchi ambaye awali hakujiandikisha, anatakiwa kufika katika ofisi za mamlaka hiyo na kuanza na hatua ya kwanza ya kujaza fomu. 
“Mwananchi anatakiwa kufika ofisi zetu za wilaya, na hapo atapewa maelezo na ataanza na hatua ya kwanza ya kujaza fomu, baadaye ataitwa kwa hatua ya pili ya kuchukua alama za vidole na picha,” alisema na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaweka namba za simu ambazo wanazitumia ili kutopoteza mawasiliano. 
Akizungumzia utoaji vitambulisho kwa wilaya tatu za Mkoa wa Dar es Salaam, William alisema shughuli hiyo imefikia tamati juzi.
“Kazi ya utoaji wa vitambulisho kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam tumeimaliza jana (juzi), kwa wale kwa sababu moja au nyingine wameshindwa kufika kuchukua kwenye kata wanatakiwa kwenda ofisi zetu za wilaya,” alisema.

No comments: