MTOTO AFA KWA KUANGUKIWA NA UKUTA


Watu watatu wamekufa katika matukio matatu tofauti jijini Dar es Salaam, akiwamo mtoto wa miaka mitatu, Asha Rajabu aliyeangukiwa na ukuta wa nyumba yao wakati akicheza na wenzake. 
Kamanda wa Polisi Ilala, Mary Nzuki (pichani) alisema tukio hilo ni la juzi saa 12 jioni, eneo la Kipawa wilayani IIala ambapo Rajabu alidondokewa na ukuta huo unaodaiwa ulikuwa mbovu kwa muda mrefu, mtoto alikufa papo hapo na maiti imehifadhiwa Hospitali ya Amana kwa uchunguzi. 
Katika tukio jingine, lililotokea barabara ya Morogoro eneo la Magomeni Mapipa mtu asiyefahamika aliyekadiriwa kuwa na miaka kati ya 25 hadi 30 ambaye alikuwa ni abiria wa pikipiki amekufa papo hapo baada ya pikipiki aliyokuwa amepanda kumgonga mtembea kwa miguu. 
Kamada wa Polisi Kinondoni, Camillius Wambura alisema mtu huyo alikufa baada ya pikipiki aliyokuwa amepanda iliyokuwa ikiendeshwa na dereva  asiyefahamika mwenye umri wa miaka (25-30) akiwa na pikipiki aina ya Boxer namba T 321 CRT akitokea Magomeni kwenda Fire alimgonga mtembea kwa miguu Zahoro Suleiman (25-30) ambaye alikuwa anavuka barabara. 
Alisema abiria wa pikipiki alikufa papo hapo na dereva na mtembea kwa miguu walijeruhiwa na wako katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu na maiti imehifadhiwa katika hospitali hiyo. 
Tukio la tatu lililotokea Barabara ya Nyerere eneo la Quality Center, mtu aliyefahamika kwa jina moja la Mudi anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 40 hadi 45 amekufa baada ya kugongwa na gari. 
Kamanda wa Polisi Temeke, Kihenya wa Kihenya alisema mtu huyo aligongwa na gari aina ya Nissan Saloon lenye namba za usajili T111 CWH lililokuwa likiendeshwa na Haruni Kamara (28) mkazi wa Tabata Bima ambaye alikuwa akitokea Tazara kwenda Veta.

No comments: