SMZ YAJIZATITI KUKABILIANA NA EBOLA


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza mikakati ya tahadhari kukabili ugonjwa wa ebola kwa kuweka udhibiti wa vifaa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar pamoja na Bandari Kuu ya Malindi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud aliwaambia waandishi wa habari juzi kwamba juhudi za mikakati zinahitajika kwa ajili ya kujilinda na ugonjwa huo ambao hadi sasa hauna tiba wala chanjo.
Alisema maeneo ambayo yatawekwa udhibiti pamoja na vifaa mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo ni uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume ambao umekuwa ukipokea wageni mbali mbali kutoka nje ya nchi ikiwemo watalii. 
“Tumechukua hatua zote muhimu za tahadhari kwa wageni katika maeneo muhimu ikiwemo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa kuweka vifaa vya kukabiliana na ugonjwa huo kama atapatikana mgonjwa,” alisema. 
Aidha, alisema vifaa vitawekwa katika Bandari Kuu ya Malindi inayopokea idadi kubwa ya wageni wanaotoka Tanzania Bara na baadhi ya nchi za  nje.\Aboud alisema kwa sasa elimu kuhusu kukabili ugonjwa wa ebola itatolewa kupitia vyombo vya habari mbali mbali wananchi waweze kufahamu dalili za ugonjwa huo.\Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mikakati ya kuchukua hadhari kukabili ugonjwa huo.

No comments: