MAHAKAMA YAELEZWA NJAMA ZA KUTEKA WATOTO KUJIPATIA MILIONI 300/-Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa raia wawili wenye asili ya bara la Asia walikiri kupanga njama za kuwateka watoto wawili kwa lengo la kujipatia Sh milioni 300.
Mawakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono na Janetoreza Kitali walidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka wakati wakiwasomea washitakiwa hao maelezo ya awali.
Washitakiwa hao wanaokabiliwa na kesi ya kupanga njama za kuwateka watoto wawili wa Anali Akber Haji kwa lengo la kujipatia fedha hizo ni Adil Arshad Yusuph (24) na Mehul Kava (24).
Wakisoma maelezo ya awali, mawakili hao walidai Machi 16 mwaka jana katika eneo lisilofahamika, washitakiwa walikubaliana kutekeleza mpango wa kuwateka watoto hao.
Iliendelea kudai kuwa katika kutekeleza mpango huo, washitakiwa walikodi watu kwa ajili ya kuwatekea watoto hao.
Hata hivyo, hawakufanikiwa baada ya polisi kupata taarifa na kuandaa mtego wa kuwakamata. Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Septemba Mosi mwaka huu.

No comments: