BENKI YA POSTA, LAPF KUTOA MIKOPO KWA WASTAAFUBenki ya Posta Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Pensheni wa LAPF, wamezindua mpango maalumu wa kutoa mikopo kwa wastaafu.
Akizungumza katika uzinduzi huo jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi alisema wameamua kuanzisha aina hiyo ya mkopo baada ya kugundua kwamba wastaafu wamekuwa wakipata taabu kupata mikopo kutoka kwenye taasisi nyingi za kifedha hapa nchini.
“Mkopo huu ni wa kwanza wa aina yake katika soko la benki hapa nchini na tunaamini utampa amani mwanachama wa LAPF ambaye amestaafu na utamwezesha kuanzisha ama kuendeleza biashara yake  aweze kutimiza malengo yake na kujiongezea kipato na hivyo kuondokana na utegemezi wa ndugu au watoto,” alisema.
Alisema mstaafu anayetaka kukopa hahitaji kuwa na dhamana, na riba inayotozwa kwa mkopo huo ni ndogo ukilinganisha na mikopo mingine ambayo ni asilimia 12 kwa mwaka.
Alisema mkopo umewekewa bima, hivyo endapo mkopaji atafariki familia yake haitaendelea kudaiwa.
Akizindua mpango huo, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka alisisitiza wastaafu wenye sifa za kuomba mikopo hiyo, kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo  waweze kujiendeleza kimaisha, kwani wakiitumia vizuri mikopo hiyo itakuwa chachu ya maendeleo yao na kuishi maisha ya faraja.

No comments: