VYUO VITANO VYA UANDISHI KUTUMIA MITAALA YA NACTEBaraza la Habari Tanzania (MCT), limetoa idhini ya kudumu kwa vyuo vitano vya uandishi wa habari katika ngazi ya cheti na Stashahada, kutumia mitaala ya taifa iliyothibitishwa na Baraza la Elimu ya Ufundi (Nacte).
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendanji wa MCT, Meneja Machapisho, Utafiti na Uhifadhi Hati wa baraza hilo, John Mirenyi alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya vyuo husika kukidhi vigezo muhimu vinavyotakiwa.
“Hatua hii imefikiwa baada ya MCT kwa kushirikiana na Nacte  tulifanya ukaguzi wa vyuo hivyo mwaka huu ili kubaini uwezo wao wa kutumia mitaala hiyo,” alisema.
Mirenyi (pichani) alitaja vigezo vinavyozingatiwa ni pamoja na uwepo wa vifaa, mazingira ya taaluma, uwezo wa walimu kufundisha, miundombinu na uongozi.
Idadi hii inafanya kuwapo kwa vyuo saba nchini vilivyopewa idhini ya kudumu ya kutumia mitaala hiyo.
Vilivyopata idhini mwaka huu ni Dar es Salaam School of Journalism (DSJ), Time School for Journalism (TSJ), Royal College of Tanzania (Dar es Salaam), Chuo Kikuu wa Kiislamu cha Morogoro na Teofilo Kisanji (Mbeya).
Vingine ambavyo vilipata idhini mwaka 2013 ni A3 Institute of Professional Studies (Dar es Salaam) na Arusha Journalism Training College cha Arusha.
Aidha, Mirenyi alisema vyuo vitatu vilivyoruhusiwa kutumia mitaala kwa muda, vimeongezewa muda wa miezi sita vikamilishe vigezo vinavyotakiwa. Vyuo hivyo ni Kyela Polytechnic College (Mbeya), Institute of Social and Media Studies (Arusha), na Morogoro School of Journalism (Morogoro).
Alisema Chuo cha City Media College cha Arusha hakijaruhusiwa tena kutumia mitaala hiyo, kutokana na kutoomba kufanyiwa ukaguzi  kubaini uwezo wake, ingawa mwaka jana kiliruhusiwa kwa muda.

No comments: