KIU CHATANGAZA UDHAMINI KWA WANAFUNZI 1,800Chuo cha Kimataifa cha Kampala (KIU) kimetangaza kutoa udhamini kwa wanafunzi 1,800 watakaojiunga kuanzia mwaka huu wa masomo kwa kuwalipia nusu ya ada.
Mpango huo wa udhamini ambao umetajwa kuwa endelevu, umeelezewa na uongozi wa chuo kwamba utakigharimu takribani Sh bilioni 2.5 kila mwaka kuutekeleza.
KIU ambacho kimetoa nafasi 10 kwa kila wilaya kwa wanafunzi watakaojiunga nacho na kufanya idadi ya wadhaminiwa kufikia 1,800, pia kimeshusha ada kutoka Sh milioni 2.8 hadi Sh milioni 1.6 kwa masomo ya jamii.
Uongozi wa chuo hicho ulitoa taarifa hiyo jana Dar es Salaam  kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari na kusema ni mkakati wake wa kuhudumia jamii ya Watanzania.
Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Muhammad Ndaula alisema udhamini wa chuo hicho chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 6,000 mwaka huu, utazingatia ufaulu pamoja na wanafunzi wasio na uwezo kiuchumi.
Alisema kwa kuwa wanafanya kazi kwa karibu na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) pamoja na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Heslb), alisema vigezo vya bodi katika kutoa mkopo pia vitasaidia wao kubaini wanafunzi wenye uhitaji.
“Mpango unaanza sasa na ni endelevu,” alisema Profesa Ndaula na kufafanua kwamba kwa wanaochukua kozi za miaka mitatu, udhamini ni kwa asilimia 50 na kwa wenye kozi za miaka minne watadhaminiwa kwa asilimia 40.
Kuhusu kupunguza ada, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano, Thomas Somme alisema baada ya kuona Watanzania wengi wanashindWa kupata elimu kwa sababu ya ada kubwa, wameamua kupunguza kwa kiwango hicho kikubwa.
Alipoulizwa kama upunguzaji ada ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa TCU wa ada elekezi kwa vyuo, Somme alisema wamezingatia mantiki ya biashara pamoja na utoaji huduma kwa jamii.
Machi mwaka huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alizindua mfumo wa gharama halisi za vyuo vikuu nchini ulio chini ya TCU. Alitaka taasisi za elimu ya juu kutafuta vyanzo vingine vya fedha badala ya kutegemea serikali na ada.

No comments: