RITA YABAINI UDANGANYIFU VYETI VYA KUZALIWAWakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umebaini udanganyifu uliofanywa na walimu wa shule za msingi na wazazi kughushi taarifa na kuongeza bei wakati wa kusajili na kuwapatia wanafunzi vyeti vya kuzaliwa.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu  wa Rita, Philip Saliboko (pichani) wakati wa uzinduzi wa utekelezaji mkakati wa usajili na kuwapatia vyeti wanafunzi wa sekondari uliofanyika jijini hapa.
Alisema ni vyema walimu wakaweka uzalendo mbele na kufuata maelekezo ya utoaji nyaraka kama watakavyofundishwa na kuepuka vitendo vya udanganyifu kama vilivyofanywa na baadhi ya walimu wa shule za msingi.
Aliongeza kuwa Rita kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala inategemea kuanza uandikishwaji kwa shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam na utafanyika chini ya mkakati wa usajili wa watoto walio na umri kati ya miaka 6-18 kwani watoto wengi wapo kwenye kundi hilo.
“Jumla ya shule za sekondari 96 zitashiriki katika mkakati huu zenye jumla ya wanafunzi 53,028 na lengo ni kusajili na kutoa vyeti kwa wanafunzi 15,000,” alisema Saliboko na kufafanua kuwa walimu watakusanya ada za vyeti kwa kila mtoto ya Sh 10,000 tu.
Ofisa Elimu Msaidizi Manispaa ya Ilala, aliyekuwa mgeni rasmi Epifania Mtumbuka alisema wazazi wanatakiwa kupeleka watoto wao kusajiliwa ili mtoto akimaliza kidato cha sita na akipata nafasi ya kwenda nje awe na cheti cha kuzaliwa.

No comments: