KAMATI KUU CCM KUJADILI BUNGE KATIBAMwenyekitiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete jana alifungua kikao maalumu cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, ambapo pamoja na mambo mengine kitajadili mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba.
Akifungua kikao hicho jana, Rais Kikwete alisema hana ajenda za kikao hicho mfukoni, lakini wamekutana kwa lengo la kuzungumza mambo yanayoendelea.
“Sina ajenda mfukoni tumekutana tuzungumze mambo yetu,” alisema na kufafanua kuwa mara ya mwisho kukutana ilikuwa Julai na safari hii wamekutana ili kuangalia mambo ya chama yanavyoendelea, na kufanya  uamuzi ili waendelee mbele.
Awali Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema kikao hicho ni maalumu na mpaka kinafunguliwa jana, wajumbe 33 kati ya 34 walikuwa ukumbini na mjumbe ambaye hakuweza kufika alikuwa, Jerry Silaa.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kufunguliwa kwa kikao hicho, Katibu NEC wa Itikadi na Uenezi, Nnape Nnauye, alisema moja ya ajenda katika kikao hicho ni kujadili mchakato mzima wa Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea.
Pia alitoa mwito kwa waandishi wa habari kuandika habari kutoka chombo husika na sio kuokota taarifa barabarani na kuonya kuwa atakayekiuka hilo atachukuliwa hatua.
Alisema taarifa nyingi zinazoandikwa kwenye magazeti si za kweli na kuwataka waandishi kutafuta ufafanuzi na si kufikiria tu kufanya biashara ya kuuza magazeti. “Tusifanye biashara na maisha ya nchi,” alisema Nape.

No comments: