WAPANDISHWA KORTINI KWA KUINGIZA MAGAIDI NCHINIViongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, wanakabiliwa na mashitaka ya kuingiza wageni nchini, ili washiriki katika vitendo vya kigaidi.
Jana kiongozi mwandamizi wa Jumuiya  hiyo, Mselem Ali Mselem, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka hayo.
Mselem na Abdallah Said Ali, walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Peter Njike akisaidiwa na Wakili George Barasa, mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.
Mselem amepandishwa kizimbani, baada ya kiongozi mwenzake mwandamizi katika jumuiya hiyo, Farid Hadi Ahmed, pamoja na washitakiwa wengine 19,  kufikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na tuhuma za kujihusisha na vitendo hivyo.
Wakili Barasa alidai, katika tarehe tofauti nchini, kati ya Januari mwaka jana na Juni mwaka huu, washitakiwa walipanga njama za kutenda kosa la kuwaingiza watu nchini kwa ajili ya kufanya ugaidi.
Ilidaiwa katika kipindi hicho, huku washitakiwa wakijua kuwa ni kosa, walikubali kuwaingiza watu nchini kwa ajili ya kujihusisha na vitendo hivyo.
Katika mashitaka yanayomkabili Mselem, Wakili Barasa alidai, mshitakiwa aliwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omary ili washiriki katika vitendo vya ugaidi, ingawa hakusema wanatoka nchi gani.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi haujakamilika na kuomba kesi hiyo itajwe kesho na Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi itakapotajwa tena.

No comments: