NDEGE ZISIZO NA RUBANI KUFICHUA UJANGILI ZAJA


Kampuni ya Bathawk Recon inafanya mazungumzo na Wizara ya Maliasili na Utalii, ya kuleta teknolojia ya ndege zisizo na rubani, kwa ajili ya kufichua majangili wanaoua wanyama katika hifadhi za Taifa.
Ndege hizo aina ya UAV, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Tom Lithgow, zinaendeshwa bila rubani na kazi yake ni kutumwa katika hifadhi  kupeleleza kama kuna majangili yamejificha au silaha zilizofichwa katika hifadhi hizo.
Kwa mujibu wa Lithgow, ndege hizo zikishapata taarifa hizo, zinatoa taarifa kwa mamlaka za wanyama pori ambako watalazimika kuwatuma askari wa doria, kufika eneo hilo litakalokuwa na silaha au majangili watakaokuwa wamejificha.
"Teknolojia hii inatumika katika nchi zilizoendelea, tumeona Tanzania inakabiliwa na tatizo  la majangili ambao wanaua wanyama adimu duniani kama tembo, faru na wengineo, tunaamini kuwa teknolojia hii itakuwa na manufaa kwa nchi," alisema Lithgow.
Alisema ujangili unaongezeka hapa nchini kwa vile askari wa wanyama pori wanatumia vifaa duni na hawana vifaa vya kufanyia doria katika eneo kubwa, hivyo ndege hizo zitasaidia kwani kwa siku moja zinaweza kufanya doria katika mbuga yote na kutoa taarifa za kuwepo kwa majangili hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta binafsi (TPSF), Geofrey Simbeye, alisema taasisi yake imeleta kampuni hiyo kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete akiwa Marekani, aliomba mataifa yaliyoendelea yaisaidie katika kupambana na ujangili.
"Waliuliza wanataka watusaidieje katika vita hii? Sisi kama sekta binafsi tunaona kwamba teknolojia hii ni jibu la matatizo ya ujangili nchini na itasaidia kuwaokoa wanyama wanaowindwa," alisema Simbeye na kufafanua kuwa wako kampuni hiyo iko tayari kuleta ndege hiyo kwa majaribio katika mbuga ya Seronera.
Simbeye alisema kwamba sekta binafsi ina kila sababu za kuhakikisha kuwa wanyama ambao ndio kivutio kikubwa kwa watalii wanaendelea kuwepo ili kulinda ajira za watu 300,000 ambao wameajiriwa katika sekta hiyo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyama Pori katika Wizara ya Maliasili na Utalii Julius Kibebe, alisema Serikali tayari imepokea maombi ya teknolojia nyingi ambazo wanataka kutuuzia ila kasema kwa kampun ya Bathawk Recon wao wanataka kuingia ubia na Serikali.

No comments: