Zahanati ya
kijiji cha Nafuba, kilichopo katika kisiwa ndani ya Ziwa Victoria wilayani
Bunda mkoani Mara, ina mganga mmoja tu ambaye amekuwa akilazimika kuifunga
anapopata dharura na kusababisha wagonjwa kukosa huduma ya matibabu.
Mganga Mkuu
wa Zahanati hiyo Robert Magela, ameliambia gazeti ili juzi kuwa amekuwa
akifanya kazi katika mazingira hayo kuanzia mwaka 2007 na kwamba yeye alihamia
kwenye kituo hicho mwaka 2003 kukiwa na muuguzi mmoja ambaye pia baadaye
aliondoka.
Alisema kuwa
pindi anapopata dharura ama ya kuitwa wilayani kwa ajili ya kupeleka taarifa,
amekuwa akiifunga zahanati hiyo hali ambayo husababisha wagonjwa kukosa huduma
ya matibabu, wakiwemo akinamama wajawazito wanaotaka kujifungua.
“Nimefanya
kazi hii nikiwa mwenyewe tangu mwaka 2007…nafanya huduma zote mimi mwenye na
ninapopata dharura nimekuwa nikilazimika kuifunga, hali ambayo husababisha
wagonjwa kukosa huduma” alisema.
Alisema
zahanati hiyo inahudumia wananchi zaidi 4,493, wakiwemo wagonjwa kutoka katika kisiwa hicho na kisiwa kingine
jirani cha Sozia, ambapo wakazi wake wengi ni wavuvi na wafabiashara wa kutoka
katika mikoa yote ya kanda ya ziwa.
Aidha,
alisema kuwa hali hiyo imekuwa ikimfanya asipate nafasi ya kupumzika, kwani
hali ya magonjwa katika kisiwa hicho iko juu, kulingana na mazingira halisi
yalivyo visiwani humo, ambapo baadhi ya kaya hazina vyoo.
Mganga huyo ameiomba serikali pamoja na mashirika
yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulika na masuala ya ukimwi kufika katika
visiwa hivyo, ili waweze kutoa elimu kwa jamii juu ya maambukizi ya ukimwi na
jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo hatari, badala ya elimu hiyo kuitoa sehemu za
mjini tu.
No comments:
Post a Comment