ASILIMIA 23 YA WENYE UMRI WA KUZAA WANA UZITO ULIOKITHIRI


Zaidi  ya asilimia 23 ya wanawake wenye umri wa kuzaa, wamegundulika kuwa na uzito uliokithiri ambao pamoja na athari za kiafya, kwa upande wa wajawazito unahatarisha afya kwa mtoto anayezaliwa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka alisema hayo wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu inayohusisha wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa (UN), sekta binafsi na wadau mbalimbali wa masuala ya lishe nchini.
Kwa mujibu wa Dk Turuka, uzito uliokithiri kwa wanawake licha ya kuwaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo, wakati mwingine inaweza kusababisha kuzaliwa kwa watoto wenye uzito mdogo.
Hali hiyo ya uzito uliokithiri, imetajwa kusababishwa na matumizi ya vyakula vyenye protini kwa wingi bila ya kufanya mazoezi pamoja na mifumo ya maisha waliyojiwekea wanawake.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Profesa Joyce Kinabo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), alisema matumizi ya vyombo vya usafiri hususani magari ni miongoni mwa mambo yanayochangia uzito uliokithiri.
“Unakuta wanawake wakitoka nyumbani wanapanda kwenye magari yao hadi ofisini, wakishamaliza kazi zao wanapanda magari kurudi nyumbani bila kufanya mazoezi mengine,” alisema Profesa Kinabo.
Katika hatua nyingine,  semina hiyo ilielezwa asilimia 53 ya wanawake wenye ujauzito wana matatizo ya upungufu wa damu kutokana na lishe duni.
Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo aliwaasa wanawake wajawazito kuzingatia lishe bora kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanakuwa na afya bora.

No comments: