KESI YA VIPIMO BANDIA VYA HIV YAPIGWA KALENDA


Kesi ya kuingiza nchini vipimo bandia vya kupima virusi vya Ukimwi (HIV)  na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni tatu, inayowakabili vigogo wawili wa Bohari ya Dawa (MSD) na wenzao imeahirishwa hadi Septemba 4 mwaka huu.
Hakimu Mkazi Augustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo jana kwa kuwa Hakimu Mkazi Hellen Liwa anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo.
Awali Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Leonard Swai alidai washitakiwa waliambiwa wasifike mahakamani jana isipokuwa Mkurugenzi wa Operesheni Kanda ya Kaskazini wa Bohari ya Dawa (MSD), Sylvester Matandiko.
Alidai kuwa, mara ya mwisho kesi ilipotajwa mahakama ilitoa amri Matandiko ambaye anaumwa afikishwe mahakamani au akasomewe mashitaka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Upande wa utetezi ulidai mshitakiwa bado anaumwa na yupo tayari kwenda kusomewa mashitaka hospitali.  Hakimu Mmbando alikubali kwenda kumsomea mashitaka huko lakini baadaye aliahirisha kesi na kusema Hakimu Liwa ndiye atakayeendelea kuisikiliza.
Mbali na Matandiko, washitakiwa wengine ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa MSD, ambaye pia ni Meneja wa Viwango, Sadiki Materu na wasajili kutoka Bodi ya Maabara za Afya, Zainabu Mfaume na Joseph Nchimbi.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka saba: ya kula njama, kutumia madaraka vibaya, kuingiza vipimo bandia vya HIV na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni tatu.
Matandiko anadaiwa Februari 3, mwaka juzi, katika ofisi za MSD Temeke, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuruhusu Bodi ya Maabara za Afya kutoa kibali kwa Kampuni ya SD Africa, kuingiza vipimo bandia vya HIV vilivyotengenezwa na Kampuni ya Standard Diagnostics ya Korea, vilivyozuiliwa na Serikali kuingizwa nchini hivyo kusababisha hasara hiyo.

No comments: