WIZARA YATISHIA KUIFUTA SHULE YA MKOREA

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imetishia kuifutia usajili shule ya kimataifa ya Eden iliyopo Chukwani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,  kwa madai ya kubainika kutoa mafunzo ya Biblia kwa wanafunzi wa shule ya msingi kinyume na utaratibu.
Mrajisi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo, Siajabu Suleiman Pandu alisema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake  mjini hapa, baada ya kujitoleza malalamiko kutoka kwa wazazi kuhusu mwenendo wa shule hiyo.
Pandu alisema shule hiyo, inamilikiwa na Shirika la Kimataifa la African Agape Association, chini ya mwekezaji kutoka Korea, aliyejulikana kwa jina la Pil-Soon-Youn.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Namba 6 ya mwaka 1986, Shule zilizosajiliwa zipo huru  kusomesha masomo ya dini, lakini hazitakiwi kulazimisha wanafunzi.
Alisema  kwa mujibu wa kifungu cha 47 hadi 48 cha Sheria hiyo,  shule zitakuwa zikitoa elimu na mafundisho ya dini kwa wanafunzi wake,  lakini mafundisho hayo yapate ridhaa kwa wahusika, wakiwemo wazazi na siyo kwa kulazimisha.
“Katiba zote mbili zinatamka wazi uhuru wa kuabudu kwa wananchi wake na hata sheria ya Wizara ya Elimu imeweka bayana shule au taasisi kutoa mafunzo ya dini lakini si kwa njia ya kuwalazimisha wanafunzi wake,” alisema.
Alisema mafundisho ya dini yatatolewa bila ya masharti, lakini kwanza yanatakiwa kuzingatia imani za wanafunzi inayowahusu na siyo kwa njia za kulazimishwa.
Akizungumzia umiliki wa shule hiyo chini ya mwekezaji huyo wa Korea, Pandu alisema, “Huyu mmiliki wa shule ameingia nchini kama mwekezaji na kusajiliwa na Shirika lake la Agape na Mamlaka ya Vitega uchumi Zanzibar  (ZIPA)”.

No comments: