RAIA WA ZAMBIA AKUTWA AMEKUFA HOTELINI DAR

Watu wanne wamekufa katika matukio tofauti, ikiwamo raia wa Zambia, Bryton Chimidu (45) aliyekutwa amekufa ndani ya hoteli ya Jangwani Sea Breeze chumba namba 217.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema tukio hilo ni la juzi saa 4 asubuhi katika hoteli hiyo iliyopo wilayani Kinondoni.
Alisema raia huyo wa Zambia, alikuwa na pasipoti namba CN 825873,  iliyotolewa na Jamhuri ya Zimbabwe. Alisema Chimidu alikutwa amekaa sakafuni huku ameegemea ukuta pembeni ya mlango, akiwa hana nguo.
Kwa mujibu wa Wambura, kwenye meza ndani ya chumba hicho kulikutwa dawa, chupa tatu za pombe  kali aina ya Peronenastroo azzuro na kopo tupu la Redbull. Maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Katika tukio jingine, mkazi wa Kisota ambaye jina lake halikufahamika, amekutwa amejinyonga kwa kutumia kamba za turubai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema tukio hilo ni la juzi saa 12 alfajiri maeneo ya Kisota wilayani humo. Alisema mtu huyo inadaiwa alikuwa akiishi na familia yake na kwamba alikuwa na tabia ya ulevi.
Kwa mujibu wa Kiondo, marehemu alikuwa akigombana na mkewe mara kwa mara kutokana na ulevi huo.
Mwanamke aliyedaiwa kuwa mke wa marehemu Frida Somii (44) anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano  kuhusu tukio hilo. Maiti imehifadhiwa Hospitali ya Vijibweni Temeke.
Katika tukio jingine, mkazi wa Kibamba, Wille Emmanuel (35) amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari.
Kamanda Wambura alisema tukio hilo ni la juzi saa 4 usiku, katika barabara ya Morogoro eneo la Kibamba wilaya ya Kinondoni.
 Alisema gari ambalo halikufahamika namba zake, lililokuwa likitokea Mbezi kuelekea Kibaha, ilimgonga mtembea kwa miguu Emmanuel, aliyekuwa akivuka barabara na kusababisha kifo chake. Maiti imehifadhiwa Hospitali ya  Tumbi Kibaha.
Mkazi wa Mzizini, Alfas Adolf (23) naye amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili T 290 AVS aina ya Escudo katika barabara ya Pugu, eneo la Pugu Mzambarauni juzi saa 2 asubuhi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema gari hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Shomari Hassan (35) mkazi wa Tabata Kimanga, akitokea Ukonga kuelekea Pugu. Maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na dereva huyo amekamatwa.

No comments: