WAUMINI WASEMA ASKOFU MPYA KKKT NI CHAGUO LA MUNGU

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha wamesema Askofu Mteule, Mchungaji Solomon Massangwa ni chagua la Mungu.
Wamesema kwa nyakati tofauti kuwa Solomon anauwezo mkubwa wa uongozi hivyo hawana mashaka naye.
Massangwa alichaguliwa juzi jijini hapa kuwa Askofu wa dayosisi hiyo baada ya kupata kura 261 kati ya 263, sawa na asilimia 99.98. Msaaidizi wake alichaguliwa Mchungaji Gidion Kivuyo aliyepata kura 242 kati ya kura 263.
Muumini wa dayosisi hiyo, Methew Mollel alisema kuwa wajumbe waliompigia kura Massangwa wametimiza sauti ya Mungu kwa kuwa na imani kubwa na mteule huyo.
Mollel alisema waumini wana imani na utendaji wake kutokana na kipindi alichokaimu nafasi hiyo kufanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kuunganisha waumini wa kanisa hilo kuwa kitu kimoja.
“Massangwa ni chaguo la Mungu na wajumbe wamebarikiki hilo hivyo sioni sababu ya mimi kushindwa kumwamini,” alisema Mollel.
Kwa upande wake msharika wa Ngateu, Mathias Laizer alisema kuwa hana wasiwasi na utendaji kazi wa mteule huyo kwani katika kipindi cha kukaimu nafasi Askofu, ameongeza imani kwa waumini  wa ndani na nje ya dayosisi na nchi.
Naye, Josephat Lema muumini wa Usharika wa Mjini Kati, alitumia neno la mtaani kuwa Massangwa ni ‘jembe’ na wajumbe hawajakosea kumchagua.
Lema alitumia msemo wa mtaani kuwa mteule huyo ni jembe na kuwataka wajumbe wa mkutano huo na waumini wote kumpa ushirikiano.
Massangwa alichaguliwa kuchukua nafasi ya Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk Thomas Laizer aliyefariki dunia februari 6 mwaka jana mjini hapa baada ya kuugua.

No comments: