WALIOPATA DARAJA LA KWANZA KIDATO CHA NNE KUSOMESHWA BURE UALIMU

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imewahakikishia wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka huu waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na kuamua kusomea ualimu wa Sayansi ngazi ya Stashahada, watasomeshwa bure.
Pia, imesisitizwa wahitimu waliofaulu kwa daraja la pili na tatu wakaamua kusomea fani hiyo ya ualimu katika Sayansi, watapewa mkopo.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri, Jenista Mhagama katika mkutano wa hadhara mjini Namtumbo mkoani Ruvuma  baada ya Rais Jakaya Kikwete kufungua barabara ya Songea- Namtumbo na kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Namtumbo- Kilimasera- Matemanga.
Mhagama alisema,  hivi sasa wapo  wanafunzi 4,000 wanaosomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma,  na wengine wapo katika vyuo 30 vya ualimu nchini.
Alisema Serikali imeamua kuwa na mkakati maalumu wa kupata walimu wa sayansi kukabili uhaba uliopo.
Kwa mujibu wa Mhagama, Serikali itahakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kupitia kwa walimu bora.
Rais Kikwete alisema upungufu wa walimu wa sayansi ni tatizo kubwa. Lakini, alihakikishia umma kwamba Serikali itawapata.
“Tatizo letu kubwa hivi sasa ni walimu wa sayansi, Naibu Waziri wa Elimu ameeleza vizuri, tutafanikisha hilo,” alisema Rais Kikwete.

No comments: