WATOTO 125 WAONDOLEWA KWENYE AJIRA MBAYA

Watoto 125 waliofanyiwa ukatili majumbani pamoja na kutumikishwa wakiwa chini ya miaka 14 wameondolewa kwenye ajira hizo na kurudishwa makwao.
Hayo yalielezwa juzi na Mwanasheria wa Shirika la Kutetea Haki za Watoto wanaofanya kazi za majumbani la ‘Wote Sawa’, Saida Mavumbi katika mahojiano na mwandishi wakati wa kuwaondoa watoto hao.
Alifafanua kuwa watoto hao waliondolewa kwenye ajira hizo kuanzia Oktoba, mwaka jana hadi sasa ambapo 53 walikuwa wakifanyiwa ukatili na waajiri wao kwa kupigwa, kuchomwa moto na kunyimwa mishahara yao.
Alisema 72 walikuwa na umri wa chini ya miaka 14 hivyo kuondolewa na kurejeshwa kwenye familia zao na kufanyiwa mipango ya kupelekwa shule.
Kwa mujibu wa sheria ya mtoto, kifungu namba 21 ya mwaka 2009, mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 14 haruhusiwi kufanyishwa kazi za ajira.
Alisema mradi huo unatekelezwa katika kata tano za halmashauri ya Jiji la Mwanza zikiwemo za Isamilo, Igombe, Mbugani, Kirumba na Mahina lakini leseni yao haiwanyimi kufanya kazi katika maeneo mengine.
Alisema wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa, mabalozi wa nyumba kumi na dawati la jinsia katika kufanikisha kuwabaini watoto hao ambapo baadhi ya watoto wamekuwa wakikimbilia huko kutafuta haki zao.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Wote Sawa, Angel Benedict alisema lengo la kuwarejesha watoto 300 kwa mwaka wanaotumikishwa katika umri mdogo na wanaofanyiwa vitendo vya kikatili.
Alisema moja ya mikakati juu ya watoto hao ni kuwarejesha shuleni ili wasipate nafasi ya kuwa na mawazo ya kutumikishwa.
Pia familia zenye watoto wenye umri chini ya miaka 14, zimekuwa zikipewa mafunzo ya ujasiriamali na kupatiwa mitaji itakayowawezesha kufanya biashara na kuinua kipato cha familia ambacho kwa sehemu kubwa, husababisha wazazi na walezi kuwatoa watoto ili wakafanye kazi wakiwa na umri wa kwenda shule.

No comments: