RAIS SHEIN AAGIZA BONDE LA CHEJU LISIKALIWE

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameziagiza Wizara za Kilimo, Ardhi na Mazingira kuhakikisha Bonde la Mpunga la Cheju Wilaya ya Kati haligeuzwi eneo la makazi ya watu.
Dk Shein alisema hayo wakati alipozindua shule ya maandalizi ya watoto Cheju iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya watu wa Korea ya Kusini kupitia Shirika la Saemaul Undong.
Alisema ujenzi wa barabara ya Jendele hadi Unguja Ukuu Kaibona kupitia bonde la kilimo la Cheju kwa kiwango cha Lami unaweza kuwavutia wananchi kujenga nyumba na kuweka makazi ya kudumu.
Alisisitiza na kuzitaka Wizara husika kulisimamia suala hilo huku bonde la mpunga la Cheju lenye ukubwa wa hekta 12,000 likiwa linabakia kwa ajili ya madhumuni hayo.
Alisema malengo na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji mashambani hasa katika kilimo cha mpunga na kufikiya lengo ya kujitosheleza kwa chakula.
Akifafanua zaidi alisema Zanzibar ina lengo la kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka asilimia 50 hadi kufikiya tani 80,000 zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka
2016/17.
Mapema, Balozi wa Korea ya Kusini nchini, Chung Il alisema Serikali yake imejizatiti kuhakikisha kwamba inasaidia maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu pamoja na kilimo.
Alisema shule ya maandalizi ya wanafunzi itasaidia kujenga uwezo wa wanafunzi kielimu ili baadaye waweze kuongoza taifa.
Serikali ya Korea ya Kusini inasaidia mradi wa kujitosheleza kwa chakula ikiwa ni pamoja na kilimo cha mpunga.

No comments: