WATAKA MFUMO UBORESHWE KUVUTIA WAWEKEZAJI

Serikali imeshauriwa kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji katika sekta ya rasilimali zisizojadidika yakiwemo mafuta, gesi na madini ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika sekta hizo.
Baadhi ya wadau kutoka Taasisi za Sekta Binafsi nchini (TPSF) waliyasema hayo katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi nchini ambao uliwakutanisha watafiti wa mchakato wa kujadili rasilimali hizo kwa lengo la kupokea maoni yao yatakayoboresha usimamizi wake.
Walidai kwamba nusu ya wawekezaji katika migodi wameondoka na kwenda kuwekeza nchi nyingine kutokana na mfumo uliopo.
Akichangia mada katika mkutano huo, Meneja Rasilimaliwatu kutoka kampuni ya Williamson Diamond Ltd. kutoka Shinyanga, Ignas Balyoruguru alisema utata unajitokeza zaidi katika mikataba iliyopo kutokana na kutokuwepo kwa umakini katika kufanya maamuzi.
“Tusidanganyike kwamba sisi wenyewe ndio wenye madini, hivyo unapopata fursa ya kuwa na wawekezaji nchini lazima wawekewe vivutio vizuri maana tukiwaacha watakwenda nchi ambazo kuna vivutio vingi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tan Discovery, Rogers Sezinga alisema kuwa sera zilizopo ni nzuri lakini utekelezaji hakuna na hivyo kufanya kampuni nyingi za uwekezaji kwenda nje.
Mtafiti Kiongozi wa Mchakato wa Kuboresha Rasilimali zisizojadidika (TNRC), Profesa Ammon Mbelle alisema kwa sasa wananchi wanaona kama rasilimali hizo haziwanufaishi na hivyo kuona kwamba kuna tatizo katika utawala.
Alisema tayari wameshakutana na Kamati za Bunge na Wadau wa Maendeleo, asasi za kiraia na wataendelea kufanya utafiti huo katika ngazi mbalimbali hadi kwenye wilaya ambazo rasilimali hizo zinapatikana.

No comments: