HOSPITALI YA BOMBO KUWA KITUO CHA KUSAMBAZA DAMU

Idara ya Afya mkoani Tanga imeanza mchakato wa kuifanya Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo ya Bombo kuwa kituo cha kusambazia damu salama kwenda kwenye hospitali zake za wilaya.
Kwa sasa utaratibu unaotumika kwa huduma hiyo, ni kutumia kituo pekee cha Kanda ya Kaskazini kilichopo mjini Moshi, Kilimanjaro.
Kukamilika kwa mchakato huo ambao utaratibu wake unadaiwa kuwa uko katika hatua za mwisho ili kuanza, utarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wagonjwa na kuziwezesha hospitali husika zinazounda mkoa wa Tanga kutumia muda mfupi ili kupata damu hiyo.
Mfumo wa sasa unailazimu kila wilaya kutuma maombi na kusubiri kwa muda ili kupata damu hiyo kutoka katika kituo kilichopo kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Asha Mahita amebainisha hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu mipango ya mkoa ya kukabiliana na tatizo la vifo vya wajawazito kwenye kikao kazi cha watendaji wa sekta ya afya kilichofanyika mjini Lushoto.
Lengo la kikao hicho kilichojumuisha washiriki kutoka ofisi yake, za waganga wakuu wa wilaya, wenyeviti wa bodi za afya pamoja na wadau wa sekta ya afya wakiwemo Bohari Kuu ya Dawa(MSD), Mfuko wa Bima ya Afya(NHIF), WHO, Kfw, WEI na Giz lilikuwa ni  kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya afya kwa mwaka 2014/15.
Dk Mahita alitaja tatizo la upungufu wa damu salama katika benki za damu kwamba ni miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia matukio ya vifo vingi vya wajawazito na mkoani humo.
Wakichangia hoja baadhi ya wajumbe wa kikao akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Dk Dennis Ngaromba aliwataka watendaji wenzake kuepuka kutoa rufaa za ghafla hasa zinazohusu wajawazito.
Hata hivyo, Dk Ngaromba alibainisha kwamba ni kwa kutumia mbinu hizo ya kuacha kutoa rufaa za ghafla na inapolazimu basi fomu ya kutoa historia ya mgonjwa hujazwa ipasavyo umeiwezesha wilaya ya Pangani kupunguza tatizo hilo hivi sasa.
Awali, Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto mkoani humo, Dorothy Lema akiwasilisha mada alisema: “Inakadiriwa kuwa wanawake 8,000 katika ya 100,000 hupoteza maisha kila mwaka hapa nchini, ambapo mkoani Tanga peke yake ni wastani wa wanawake 225 walipoteza maisha mwaka 2013”. 

No comments: