WATEJA 500,000 WAJIUNGA NA M-PAWA

Zaidi ya wateja 500,000 wameshajiunga na huduma ya M-pawa kufikia katikati ya Julai, mwaka huu, ikiwa ni miezi michache tangu huduma hiyo ilipozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumiliki akaunti za benki.
Mbali na idadi hiyo ya wateja, amana katika akaunti za wateja nazo zimeongezeka kufikia Sh 4 bilioni na hivyo kuonesha jinsi inavyowanufaisha wananchi. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza ameyaelezea mafanikio hayo kuwa ni makubwa na yamepatikana ndani ya kipindi kifupi cha huduma hiyo mpya ya kisasa na ya kipekee hapa nchini.
“M-Pawa imepata mafanikio makubwa na ya haraka. Hili linaakisi hali halisi ilivyokuwa awali kabla ya ujio wa huduma hii kwamba Watanzania walikuwa wakihitaji fursa ya kumiliki akaunti za benki lakini walishindwa kutokana na changamoto kadhaa,” alisema Meza.
Kuhusu uwekaji akiba, Meza alisema wateja wamekuwa wakijisajili na kutumia huduma hiyo kwa kujiwekea akiba, jambo linalotoa tafsiri kuwa watu wameelewa umuhimu wa huduma hiyo katika kuweka akiba kwa ajili ya kutimiza malengo yao.
Alisema wananchi wameonesha jinsi walivyo na dhamira ya kutimiza malengo yao ya kimaisha na kwamba kupitia M-Pawa kila mmoja atatimiza malengo yake huku akitoa rai kwa wale ambao bado hawajajiunga kufanya hivyo.
Alisema kwa ushirikiano na Benki ya Commercial Afrika (CBA), wamewapatia watu njia iliyo bora ya kumiliki akaunti ya benki kupitia simu zao za mkononi.
Ili kufungua akaunti ya M-Pawa mteja aliyesajiliwa na huduma ya M-Pesa anapaswa kupiga *150*00# na kuchagua nambari tano kwenye menu ya M-pesa ambayo ni huduma ya M-pawa na kuendelea kufuata na maelekezo.

No comments: