HIVI NDIVYO KAHABA WA TANZANIA ALIVYOSAMBAZA UKIMWI MAKUSUDI

Mwanamke mmoja wa Kitanzania aliyefanya ukabaha kwa miaka 18 katika miji mbalimbali ya Tanzania, likiwemo Jiji Kuu la kibiashara la Dar es Salaam na mingine ya Namibia, ameibuka na kueleza jinsi alivyotenda dhambi ya kusambaza Ukimwi kwa wanaume wakware.
Licha ya kukiri kufanya hivyo, akisema kwa siku alipanga hadi wanaume watano,tena bila ya kutumia kinga akisema alidhamiria kuusambaza ugonjwa huo hatari alioambukizwa akiwa katika shughuli za ukahaba. Alijigundua ameathirika mwaka 2006.
Hata hivyo, katika maelezo yake ameelezea kuijutia dhamira yake hiyo, akisema alisambaza kutokana na hasira aliyokuwa nayo dhidi ya mwanamume aliyemwambukiza.
“Nilimchukia sana kila mwanamume, yeyote aliyejiita mwanamume…nilishindwa tu kuwawinda na kuwaua, lakini dhamira yangu ilikuwa kutumia silaha yoyote kuua wanaume kwa sababu mmoja wao aliniua…
“Ndani mwangu nilijisemea kamwe sitawaambia hali ya afya yangu, yeyote anayekuja kwangu nammaliza. Kwa namna walivyoambukiza lazima niwaambukize’. Sijui nimewaambukiza wanaume wangapi, lakini ni maelfu,” alisema mwanamke huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 32, alipotoa ushuhuda wake kanisani nchini Nigeria hivi karibuni.
 
SIMULIZI KAMILI:
Ni simulizi la kutisha na kusikitisha linaloonesha chuki ya mwanamke kwa wanaume baada ya kuambukizwa virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini (Ukimwi).
“Nilimchukia sana kila mwanaume, yeyote aliyejiita mwanaume…nilishindwa tu kuwawinda na kuwaua, lakini dhamira yangu ilikuwa kutumia silaha yoyote kuua wanaume kwa sababu mmoja wao aliniua” anasema mwanamke Mtanzania aliyefanya biashara ya ngono kwa miaka 18 kwenye miji mikubwa Tanzania hasa jijini Dar es Salaam na Windhoek, nchini Namibia.
“Ndani mwangu nilijisemea, ‘kamwe sitawaambia hali ya afya yangu, yeyote anayekuja kwangu nammaliza. Kwa namna walivyoambukiza lazima niwaambukize’. Sijui nimewaambukiza wanaume wangapi, lakini ni maelfu” anasema mwanamke huyo aliyetoa ushuhuda kanisani nchini Nigeria.
Mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Miss Francis, ana umri wa miaka 32, na alifanya ngono na wanaume zaidi ya watano kwa siku kwenye miji mikubwa Tanzania na nchini Namibia. Amewaeleza waumini kuwa, aliambukiza VVU kulipa kisasi baada ya kujikuta na VVU mwaka 2006.
Mwanamke huyo aliyetoa ushuhuda jijini Lagos, Nigeria alikulia kijijini nchini Tanzania, akawa anatamani kuishi maisha ya mjini, na wakati akiwa na umri wa miaka 14 aliacha shule na kujiunga na makundi ‘mabaya’, akala njama na wasichana wenzake na kutoroka kwenda Dar es Salaam na kuiacha familia yake kijijini.
“Tulivyofika jijini nilikuta wasichana wengi wakubwa kwangu waliokuwa kwenye hii biashara ya ukahaba…walinifundisha nijiweke vipi kuwavuta wanaume na kupata wateja,” anasema mwanamke huyo aliyeanza ukahaba akiwa na umri wa miaka 14.
Alipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 16 na hakufahamu ilikuwa mimba ya nani, akaamua kuitoa kwa kutumia njia za kienyeji akashindwa, akaamua kurudi kijijini kusubiri kujifungua na akajifungua salama. Hata baada ya kuwa na mtoto, alikuwa bado na hamu ya kuendelea na ukahaba. “Nilikuwa nafanya ukahaba hata wakati nanyonyesha na matokeo yake mama yangu alininyang’anya mtoto,” anasema.
Kutokuwa na mtoto kulimpa fursa ya kurudi jijini Dar es Salaam, akajiunga tena na makahaba wenzake. Miaka minne baadaye, mama yake alimtumia ujumbe kwamba, familia yao ilikuwa imepanga kumpeleka Namibia kwa shangazi yake (wa kahaba) kuiondolea aibu sanjari na kumtoa kwenye ukahaba, alikubali.
“Nilivyofika Namibia nilijiona nipo kifungoni, sikuweza kwenda kumbi za starehe, kuvuta sigara, kulewa au kukutana na wanaume, na ndiyo mambo niliyotaka kuyafanya” anasema na kubainisha kuwa, kila mara aligombana na shangazi yake na hatimaye baada ya miezi mitatu akamfukuza.
“Nilisherehekea kwa sababu nilirudi kuishi maisha kama zamani, tayari nilikuwa na kundi la marafiki makahaba, walinionesha eneo ambalo ningeweza kuwinda wanaume na kulala nao.”
Anasema, aliendelea kuishi maisha ya anasa kwenye mitaa ya Windhoek na hakuwa na mawasiliano na familia yake, biashara ya kujiuza ikashamiri hasa kutokana na ongezeko la wafanyakazi wageni jijini humo waliomfundisha pia kutumia dawa za kulevya.
“Mwaka 2006 nilijikuta nina mimba tena, sikumjua baba wa mtoto kwa sababu nilikuwa nalala na watu watano hadi sita kwa siku, nilichohitaji ni fedha nifurahi,” anasema mwanamke huyo na kuongeza kuwa, makahaba wenzake walimshawishi asitoe ujauzito huo, na ilipokuwa na umri wa miezi sita alikwenda hospitali na akapimwa vipimo kadhaa.
“Hapo ndipo nikagundua nimeambukizwa Ukimwi…kulikuwa na hii sauti iliyosema ‘sasa ni bora ufe’ anasema kwa kuwa alitambua kifo kimekaribia aliamua ‘kuondoka’ na wanaume wengi kadri ambavyo angeweza.
“Siwezi kuhesabu nimewaambukiza wanaume wangapi. Mwanamume aliponiambia tutumie kondomu, nilimwambia angalia mwonekano wangu siwezi kuwa na ugonjwa kama huo kwa hiyo mwanamume akaishia kuniamini, ni maelfu” anasema Francis.
Alipanua wigo wa biashara yake kupitia intaneti kwa kutumia mtandao wa kijamii wa kufuta wapenzi uitwao ‘Eskimi’, na mwaka 2013 akampata mwanamume Mnigeria aliyekuwa anatafuta mwanamke kwa ajili ya uhusiano wa kudumu.
“Yule mwanamume alivutiwa na mimi na akaniuliza namna tutakavyowasiliana, aliniambia alitaka kuja Namibia kukutana na mimi,” anasema na kubainisha kuwa, baada ya mwanamume huyo kufika walianza uhusiano wa kimapenzi, na hatimaye mwanamke huyo akapata ujauzito, na hakumweleza kama anaishi na VVU.
Anasema, baada ya kujifungua alijuta na kuamua kwenda kwa mchungaji wa Kanisa la Christ Embassy kutubu dhambi zake. “Baada ya kutubu kwa Mchungaji ambaye pia ni Mnigeria, alikutana na baba wa mtoto wangu na akamuuliza kama kweli alinifahamu.”
“Alimwambia huyu msichana ametoa ushuhuda kwangu yeye anaishi na virusi vinavyosababisha Ukimwi,” anasema na kuongeza kuwa, baada ya yule mwanamume kuekelezwa vile alipoteza fahamu akakimbizwa hospitali. Inadaiwa kuwa, baada ya kupata nafuu yule mwanamume alimkimbia Francis, akahamia Angola, wakati huo mtoto wao alikuwa anakaribia miezi tisa.
Wakati huo maisha yalikuwa magumu kwa mwanamke huyo, hakupata fedha na alichoka kufanya ukahaba, akazungumza na mwanamume wake Mnigeria wakaafikiana. “Alisema, kitu pekee ambacho angenifanyia ni kunipa fedha niende Nigeria nikamwache mtoto kwa wazazi wake.”
Wakati hayo yanaendelea, wiki kadhaa kabla, rafiki yake alimweleza kuhusu uwepo wa kituo cha televisheni ya Kikristo, Emmanuel TV, kilichokuwa kinapata umaarufu nchini Namibia. Kituo hicho cha nchini Nigeria kinaendeshwa na Mchungaji T.B Joshua. Kwa kuwa alielezwa aende Nigeria kumwacha mtoto, alifanya hivyo, akamwacha mwanawe kwa wazazi wa mwanamume kwenye Jimbo la Enugu, na akatumia fursa hiyo kwenda katika Kanisa la T. B Joshua jijini Lagos.
“Nilivyofika Lagos niliwekwa kwenye gari na kupelekwa moja kwa moja kwenye Jimbo la Enugu, nilikaa pale kwa wiki moja na baadaye nikaanza kutafuta Synagogue (kanisa).” anasema.  Kwa mujibu wa Miss Francis, Aprili 27 mwaka huu alikuwa miongoni mwa waumini wengi waliokuwa katika Kanisa liitwalo Church Of All Nations (SCOAN) jijini Lagos, na ulipofika muda wa maombi, alikuwa na shauku ya kutubu.
“Kabla mwanamume mwenye busara, Christopher,  kunikaribia nilisikia kama umeme unaugawa mwili wangu na nikaanza kutetemeka. Sikujua nini kilitokea aliponiombea,” anasema. Inadaiwa kuwa, kwa sababu ya maombi hayo, mwanamke huyo aliponywa na kuondokana na mapepo yaliyomshinikiza atumie maisha yake kufanya ukahaba.
Jumapili iliyofuata, Mei 4 mwaka huu, Miss Francis alitoa ushuhuda hadharani kanisani kuhusu namna alivyofanya biashara ya kuuza mwili wake kwa miaka 18, akaambukiza VVU na yeye kuwaambukiza wanaume wengi.
“Nipo hapa kupiga magoti na kuiomba dunia yote, kila mwanamume niliyekuwa naye anisamehe”, alisema huku akilia. Amesema, baada ya kuponywa, kwa mara ya kwanza alianza kujutia vitendo vyake na akawatumia ujumbe makahaba wenzake.
“Kwenye ukahaba hakuna faida, mwisho wa ukahaba ni mchungu na wa majonzi, nawashauri vijana, kama upo kwenye hali hiyo nilipokuwa, ngoja niwe mfano machoni mwako, acha mara moja aina hiyo ya maisha, itafute sura ya Mungu,” anasema kanisani.
Miss Francis alikaa kwa wiki moja kwenye Kanisa la T.B Joshua, na baada ya hapo, mchungaji huyo akampa Dola 1,500 za Marekani (Sh milioni 2.4) za kuanzia maisha nchini Namibia. “Kamwe sitarudi kwenye ukahaba, Namshukuru sana Mungu,” anasema.

No comments: