HATUFIKIRII VITA NA NCHI JIRANI, ASEMA KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete amesema kamwe Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano kati yake na Malawi kuhusu mpaka kati ya nchi hizo, huku akiongeza kuwa, Tanzania haioni mantiki ama busara yoyote kuingia vitani na nchi yoyote jirani kwa sababu yoyote ile.
Alitoa uhakikisho huo kwa Malawi na nchi nyingine jirani wakati alipohutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa mjini Mbamba Bay, Mji mkuu wa Wilaya mpya ya Nyasa, juzi. Mji huo uko kwenye pwani ya Ziwa Nyasa.
Rais Kikwete ambaye alikuwa anasemea juhudi za kutafuta ufumbuzi wa suala la mpaka kati ya Tanzania na Malawi, alisema: "Nataka kuwatoeni wasiwasi. Hakuna sababu ya vita. Laleni usingizi bila wasiwasi, kuleni samaki wenu kwa sababu Tanzania haioni busara ya vita."
"Tanzania haiwezi kutumia nguvu kupata suluhisho la mvutano wa mpaka. Tuna uwezo wa kupata jawabu la tatizo hilo bila kutumia njia ya vita.  Tanzania haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya majadiliano. Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi pekee bali kwa mipaka yote ya Tanzania," alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia ameelezea juhudi ambazo zimekuwa zinafanywa na Tanzania kutatua tatizo hilo la mpaka ikiwa ni pamoja na kuliomba jopo la Marais wastaafu kusaidia kutafuta jawabu la mpaka kati ya nchi hizo mbili. Marais hao Joachim Chissano wa Msumbiji, Festus Mogae wa Botswana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini wanasaidiwa na jopo la Kimataifa la mabingwa wa Sheria katika kazi yao hiyo.
Rais pia amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuwa ahadi na mpango wa Serikali kununua na kuweka meli mpya katika Ziwa Nyasa uko pale pale na kwamba mipango inafanywa ya kuhamisha chelezo cha kujengea meli kutoka Mwanza kwenye Ziwa Victoria kuipeleka Itungi, Kyela, Mbeya ili kuanza ujenzi wa meli hiyo.
Rais ambaye katika Kampeni ya Uchaguzi Mkuu Mwaka 2010 aliahidi ununuzi wa meli tatu za kutoa huduma katika maziwa makuu ya Tanzania ya Victoria, Tanganyika na Nyasa amesema kuwa kiasi cha Sh bilioni 23 zimetengwa tayari kwa ajili ya kuanza ujenzi wa meli hiyo.
Amesema kuwa michoro ya meli hiyo ya Ziwa Nyasa imelazimika kubadilishwa kidogo kwa sababu ya ukweli kuwa ziwa hilo lina mawimbi makali na huchafuka mara kwa mara tofauti na maziwa Victoria na Tanganyika.
Rais Kikwete pia amewaambia wananchi kuwa Serikali inaendelea na mipango ya kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay ili kuzidi kufungua ukanda wa Mtwara na kuweza kubeba chuma na makaa ya mawe kutoka Liganga na Mchuchuma, maeneo yaliyoko katika Mkoa wa jirani wa Njombe na wilaya jirani za Nyasa na Ludewa katika Mkoa huo wa Njombe.
Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara, Rais Kikwete ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma, Rais Kikwete alikuwa na shughuli nyingi katika Wilaya ya Nyasa ambako amezindua Daraja la Ruhekei lililoko katika Kijiji cha Mkalole, kilomita nane kutoka mjini Mbamba Bay.
Alisema ujenzi wa daraja hilo ambalo lina sehemu tatu limejengwa kisasa kabisa ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga, Wilaya ya Mbinga kwenda Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa.
"Ni kweli Mwaka 2005 wakati wa kampeni ya Uchaguzi Mkuu nilishindwa kuvuka hapa kwa sababu daraja lilivunjika lakini ujenzi huu wa kisasa ni kwa sababu tunajiandaa kujenga barabara ya lami kuunganisha Mbinga na Mbamba Bay," Rais Kikwete amewaambia wananchi kwenye daraja hilo.
Rais Kikwete pia ameweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya ya Nyasa katika Kijiji cha Kilosa kilichoko karibu na Mbamba Bay na amezindua usambazaji wa umeme katika vijiji vya Wilaya ya Nyasa. Rais Kikwete anaendelea na ziara yake mkoani Ruvuma.

No comments: