IDD EL FITRI KUSWALIWA KITAIFA DAR

Wakati Waislamu wakiwa ukingoni mwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, imefahamika kuwa, maadhimisho ya kitaifa ya Sikukuu ya Idd el Fitr yatafanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yalisemwa juzi na Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum wakati wa futari iliyoandaliwa na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda kwa wananchi wa Manispaa yake, viongozi wa dini na Serikali walioko Dar es Salaam.
Kwa mara ya mwisho, Mkoa wa Dar es Salaam ulipewa hadhi ya kuwa mwenyeji wa sherehe hizo kitaifa mwaka 2010.
Akizungumza, alisema: “Nitumie fursa hii pia kutangaza rasmi kuwa mwaka huu sisi (Dar es Salaam) ndiyo tutakaokuwa wenyeji wa Swala ya Idd el Fitr kitaifa ambayo itaswaliwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja na Rais Jakaya Kikwete ndiye anayetarajiwa kuwa mgeni Rasmi. Hivyo niwaombe Waislamu kuja kwa wingi kujumuika katika  ibada hiyo itakayoanza saa moja kamili asubuhi.”
Wakati huo huo Meya wa Manipaa ya Kinondoni, Mwenda aliwataka wakazi wa Manispaa yake na nchini kote kuwasaidia watoto yatima na wasiojiweza ili kupunguza tatizo la watoto wa mitaani na yatima ambao wamekuwa wakiongezeka kila siku Dar es Salaam.
Naye Shehe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Bin Simba aliitaka Manispaa hiyo kuendeleza moyo wake wa kukutanisha watu wa rika na makundi mbalimbali katika futari na kusema ni jambo linalodumisha umoja wa Watanzania.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki aliitaka Manispaa hiyo kutumia kipindi hiki cha kiangazi kuelekeza nguvu katika kukarabati miundombinu ya barabara iliyokuwa imeharibiwa na mvua zilizopita ili kufanya sehemu zilizokuwa hazipitiki sasa kuanza kupitika kwa urahisi.

No comments: