AHIMIZA KUSOMESHA WATOTO WENYE SHIDA

Taasisi, mashirika  ya ndani na nje ya nchi na watu binafsi, wametakiwa kuendelea kutoa michango yao kusaidia kusomesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Mwito huo ulitolewa jana na mlezi wa Diana Women Empowerment Organisation (DIWEO), Emmanuel ole Naiko jijini hapa alipokutana na viongozi wa Taasisi ya Kimataifa kutoka Marekani ya International Association of Special Education (IASE), inayoshughulika na elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika nchi za Amerika ya Kusini, Afrika na Asia.
Ole Naiko ambaye pia ni Balozi wa heshima wa Botswana nchini Tanzania, alisema umefika wakati taasisi na mashirika kuongeza jitihada za kuwasaidia watoto hao ili waweze kuishi kama jamii nyingine za kitanzania na kuondokana na dhana kuwa wametengwa.
“Watoto hawa wanahitaji msaada kutoka kwetu,” alisema Balozi Ole Naiko.
Akizungumzia taasisi hiyo alisema kuwa inachofanya ni kuangalia na kuhakikisha kuwa misaada wanayotoa inawafikia walengwa na inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Alisisitiza kuwa moja ya sifa kubwa Tanzania iliyonayo ni kutumia misaada inayoletwa na wahisani kama hao katika matumizi sahihi na kwa wakati.
Taasisi hiyo inayofanya kazi katika nchi za Bangladesh, Colombia, India, Malawi, Tanzania na Vietnam, ilianzanishwa mwaka 2005 huku ikijikita zaidi katika elimu na afya hasa kwa nchi zinazoendelea kiuchumi duniani.
Kwa upande wake, mmoja wa wawakilishi wa taasisi hiyo ya kimataifa, Mary Gale alisema DIWEO ni taasisi iliyodhamiria kuwaokoa watu waishio katika mazingira magumu na hasa watoto kupitia elimu.

No comments: