MRADI WA UCHIMBAJI MADINI YA NICKEL WASUASUA

Serikali kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge, wameitaka kampuni ya Glancore yenye umiliki wa leseni ya uchimbaji madini ya Nickel katika mgodi wa Kabanga, kuacha kusuasua katika utekelezaji wa mradi huo.
Hayo yalisemwa na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga katika makao makuu ya kampuni hiyo yaliyoko Toronto nchini Canada.
Naibu Waziri aliwaeleza watendaji hao, kuwa utekelezaji wa mradi huo wa uchimbaji madini aina ya Nickel katika eneo la Kabanga wilayani Ngara, umechukua muda mrefu kuanza.
Alisema hali hiyo imeleta shaka kwa wananchi juu ya nia ya kweli ya kampuni hiyo, kuanza uchimbaji wa madini hayo nchini.
"Wananchi walikuwa na matarajio makubwa juu ya mradi na walikuwa tayari kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa miundondombinu ya utekelezaji wa mradi na hawajaendeleza maeneo yao kwa muda mrefu,” alisema Kitwanga.
Agizo hilo la wabunge na Serikali, limekuja baada ya mtendaji wa kampuni ya Glancore, Stephen Flewelling kuueleza ujumbe huo kwamba uchimbaji wa madini ya Nickel katika mgodi wa Kabanga, unaweza kuanza kati ya mwaka 2018 na 2020.
Fleweling alieleza kuwa katika kipindi cha hivi karibu, bei ya Nickel duniani imeshuka mpaka kufikia chini ya dola za Marekani sita. Alisema wataendelea na mradi, bei itakapopanda katika soko la dunia.
Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina, aliwaambia watendaji wa kampuni ya Glancore kuwa kabla yao, mradi huo ulianza miaka ya 1970 kupitia makampuni mengine bila mafanikio.

No comments: