JAJI LILA ATEULIWA KUWA JAJI KIONGOZI

Rais Jakaya Kikwete amemteua Jaji Shabani Lila (53) kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu kuanzia leo.
Jaji Lila anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Fakih  Jundu, ambaye anastaafu kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa na  Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi Ombeni Sefue, Jaji Lila ana uzoefu wa miaka 22  katika Mahakama ya Tanzania.
Alianza kufanya kazi kwenye mahakama  mwaka 1992  akiwa  Hakimu Mkazi, Tanga na kisha kutumikia mahakama katika maeneo mbalimbali nchini kwa nyadhifa tofauti.
Mwaka  2013 na sasa kabla ya uteuzi wa Jaji Kiongozi, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Masijala Kuu, akishughulikia  uanzishwaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Ilala.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais ameridhika kuwa Lila  ni mweledi, mchapa kazi, mzalendo, mwadilifu na kwamba atakuwa msimamizi na kiongozi imara wa Mahakama Kuu na Mahakama za chini.
Rais amemshukuru Jaji Jundu kwa utumishi wake mzuri na mrefu katika Mahakama kwa  kipindi cha zaidi ya miaka mitano alichokuwa Jaji Kiongozi.

No comments: