WAPEWA SIKU 14 KUHAKIKISHA SHULE ZA MSINGI ZINA CHAKULA

Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa imetoa siku 14 kwa watendaji wa vijiji kuhakikisha shule zilizopo katika vijiji  vyao zinatoa chakula  cha mchana kwa wanafunzi na atakayeshindwa awekwe ndani kwa siku saba.
Agizo hilo lilitolewa juzi  na Kaimu Mkurugenzi  Mtendaji  wa hamashauri hiyo, Chrispin Luanda  katika mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kaengesa wilayani humo wakati wa ukaguzi  wa  utekelezaji wa Mpango wa  Matokeo Makubwa Sasa (MMMS).
Alibainisha kuwa  amelazimika  kutoa agizo  hilo  kutokana na kuwepo taarifa kuwa baadhi ya watendaji wa vijiji wamekuwa wakikwamisha utekelezaji miradi ya  maendeleo katika maeneo yao.
Kaimu Mkurugenzi  huyo  alieleza kuwa  changamoto kadhaa zinazozikabili shule za msingi wilayani humo  zinaweza kutatuliwa lakini tatizo kubwa  ni baadhi ya  viongozi wa Serikali wamekuwa hawawajibiki kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

No comments: