MADINI WAKABIDHI LESENI KWA WACHIMBAJI WADOGO

Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imekabidhi leseni mbili zenye namba 1268 na 1269 kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika Kijiji cha Ishokelahela, wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Sambamba na kukabidhi leseni hizo, pia imesitisha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo kuanzia jana hadi hapo watakapotimiza masharti ya leseni hizo ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi na kuuwasilisha serikalini pamoja na kutoa mwezi mmoja wa kuondoa mali zao.
Aidha Serikali imetoa miezi mitatu kwa wachimbaji hao kuwa wametimiza masharti hayo ya leseni yakiwemo ya mpango wa uhifadhi wa mazingira, kiasi cha dhahabu kitakachochimbwa, masoko  na ulipaji wa kodi.
Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo wakati akikabidhi leseni hizo kwa wachimbaji wadogo ambapo alisema Serikali imesikia kilio chao cha muda mrefu cha kutaka leseni ya uchimbaji badala ya kuhodhiwa na mchimbaji mmoja.
Mkuu wa Mkoa ambaye alikuwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya alisema Serikali imeridhia na kukubali leseni zigawiwe kwa wachimbaji wadogo wa Ishokelahela hivyo watimize masharti yaliyowekwa ili wasinyang’anywe na kugawiwa kwa mtu mwingine.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime  aliwaeleza wachimbaji hao kuwa kuanzia wakati huo watakuwepo hapo kulinda usalama baada ya shughuli za uchimbaji katika eneo hilo kufungwa.
Alisema waliopo nje hawataruhusiwa kurudi ndani ya mashimo na waliopo shimoni watoke ili utaratibu uweze kufuatwa kwani haiwezekani wengine wawe nje na wengine waendelee na uchimbaji mashimoni.
Leseni hizo zinawahusu wachimbaji wadogo wa vikundi vitatu vya Ishokelahela, Sinuda na Kenji ambao kwa pamoja waliunda Shirikisho lililojiita Isinka na kwamba leseni yao ya tatu ipo kwenye mchakato.

No comments: